Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

85. SURAT AL-BURUUJ

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii ni ya maliwaza na kuwapa mawaidha Waumini, na kuwatisha na kuwaonya wenye inadi. Imeanzia kwa kiapo chake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa madhaahiri yanayo onekana ya uweza wake ya kwamba wapinzani wanao waudhi Waumini watafukuzwa kwenye uwanja wa rehema, kama walivyo fukuzwa walio kwenda mwendo wao katika mataifa yaliyo tangulia. Na Sura ikaingia kusimulia kisa cha hao majabari walivyo watendea Waumini, na ikafuatiza kwa kuwapa ahadi Waumini na kuwakhofisha majeuri, na kwamba Haki katika kila zama hupingwa na wapinzani. Na kwamba Qur'ani, ambayo ndiyo mwega wa Haki, na wangaikadhibisha watu fulani, lakini hiyo iko mbali kabisa na shaka, kwa sababu hakika hiyo iko katika Lauh'un Mahfuudh, Ubao Ulio Hifadhiwa ulioko kwa Mwenyezi Mungu.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa mbingu yenye Buruji! Maelezo

2. Na kwa siku iliyo ahidiwa! Maelezo

3. Na kwa shahidi na kinacho shuhudiwa! Maelezo

4. Wameangamizwa watu wa makhandaki Maelezo

5. Yenye moto wenye kuni nyingi, Maelezo

6. Walipo kuwa wamekaa hapo, Maelezo

7. Na wao ni mashahidi wa yale waliyo kuwa wakiwafanyia Waumini. Maelezo

8. Nao hawakuona baya lolote kwao ila kuwa wakimuamini Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Msifiwa, Maelezo

9. Ambaye anao ufalme wa mbingu na ardhi; na Mwenyezi Mungu ni shaahidi wa kila kitu. Maelezo

10. Hakika walio wafitini Waumini wanaume na Waumini wanawake, kisha hawakutubu, basi watapata adhabu ya Jahannamu na watapata adhabu ya kuungua. Maelezo

11. Hakika walio amini na wakatenda mema watapata Bustani zenye mito ipitayo kati yake. Huko ndiko kufuzu kukubwa. Maelezo

12. Hakika kutesa kwa Mola wako Mlezi ni kukali. Maelezo

13. Yeye ndiye anaye anzisha na ndiye anaye rejeza tena, Maelezo

14. Naye ni Mwenye kusamehe, Mwenye mapenzi, Maelezo

15. Mwenye Kiti cha Enzi, Mtukufu, Maelezo

16. Atendaye ayatakayo. Maelezo

17. Je! Zimekuwasilia khabari za majeshi? Maelezo

18. Ya Firauni na Thamudi? Maelezo

19. Lakini walio kufuru wamo katika kukadhibisha. Maelezo

20. Na Mwenyezi Mungu nyuma yao amewazunguka. Maelezo

21. Bali hii ni Qur'ani tukufu Maelezo

22. Katika Ubao Ulio Hifadhiwa.  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani