Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

75. SURAT AL-QIYAMAH

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii tukufu inasimulia khabari za kufufuliwa watu na kuhisabiwa, na khabari za Kiyama na vitisho vyake. Kisha inampa moyo Mtume s.a.w. kuwa Qur'ani itakusanywa yote katika kifua chake, na Sura ikageuka kuwakemea hao wanao penda yapitayo njia ya duniani, wakaacha ya Akhera, na ikalinganisha baina ya nyuso za Waumini zenye kung'aa na nyuso za makafiri zilizo kunjana. Na imezungumzia pia hali ya mtu aliye mguu mmoja uko kaburini, na aliyo nayo ya upungufu katika yaliyo kuwa yakimlazimu, hata akawa kama kwamba anadhani kuwa hatahisabiwa yeye. Na mwishoe Sura imekhitimisha kwa dalili zinazo pelekea lazima tuamini kuwa kufufuliwa kupo.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Ninaapa kwa Siku ya Kiyama! Maelezo

2. Na ninaapa kwa nafsi inayo jilaumu! Maelezo

3. Anadhani mtu kuwa Sisi hatutaikusanya mifupa yake? Maelezo

4. Kwani! Sisi tunaweza hata kuziweka sawa sawa ncha za vidole vyake! Maelezo

5. Lakini mtu anataka tu kuendelea na maasi kwa siku zilioko mbele yake. Maelezo

6. Anauliza: Lini itakuwa hiyo Siku ya Kiyama? Maelezo

7. Basi jicho litapo dawaa, Maelezo

8. Na mwezi utapo patwa, Maelezo

9. Na likakusanywa jua na mwezi, Maelezo

10. Siku hiyo mtu atasema: Yako wapi makimbilio? Maelezo

11. La! Hapana pa kukimbilia! Maelezo

12. Siku hiyo pa kutua ni kwa Mola wako Mlezi tu. Maelezo

13. Siku hiyo ataambiwa aliyo yatanguliza na aliyo yaakhirisha. Maelezo

14. Bali mtu ni hoja juu ya nafsi yake. Maelezo

15. Na ingawa atatoa chungu ya udhuru. Maelezo

16. Usiutikisie huu wahyi ulimi wako kwa kuufanyia haraka. Maelezo

17. Hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha. Maelezo

18. Tunapo usoma, basi nawe fuatiliza kusoma kwake. Maelezo

19. Kisha ni juu yetu kuubainisha. Maelezo

20. Hasha! Bali nyinyi mnapenda maisha ya duniani, Maelezo

21. Na mnaacha maisha ya Akhera. Maelezo

22. Zipo nyuso siku hiyo zitao ng'ara, Maelezo

23. Zinamwangallia Mola wao Mlezi. Maelezo

24. Na zipo nyuso siku hiyo zitakao kunjana. Maelezo

25. Zitajua ya kuwa zitafikiwa na livunjalo uti wa mgongo. Maelezo

26. La, hasha! (Roho) itakapo fikia kwenye mafupa ya koo, Maelezo

27. Na pakasemwa: Nani wa kumganga? Maelezo

28. Na mwenyewe akajua kwa hakika kuwa huko ndiko kufariki; Maelezo

29. Na utapo ambatishwa muundi kwa muundi, Maelezo

30. Siku hiyo ndiyo kuchungwa kupelekwa kwa Mola wako Mlezi! Maelezo

31. Kwa sababu hakusadiki, wala hakusali. Maelezo

32. Bali alikanusha, na akageuka. Maelezo

33. Kisha akenda kwa ahali zake kwa matao. Maelezo

34. Ole wako, ole wako! Maelezo

35. Kisha Ole wako, ole wako! Maelezo

36. Ati anadhani binaadamu kuwa ataachwa bure? Maelezo

37. Kwani hakuwa yeye tone ya manii lilio shushwa? Maelezo

38. Kisha akawa kidonge cha damu, tena Mwenyezi Mungu akamuumba na akamtengeneza vilivyo. Maelezo

39. Kisha akamfanya namna mbili, mwanamume na mwanamke. Maelezo

40. Je! Huyo hakuwa ni Muweza wa kufufua wafu? Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani