Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

72. SURAT AL-JINN

(Imeteremka Makka)

 

Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuamrisha Mtume wake s.a.w. katika Sura hii tukufu awafikishie watu aliyo funuliwa yeye kwa wahyi, kwamba majini wameisikiliza Qur'ani na wameitikia wito wake, na kuwapa khabari kwa yaliyo wapata wapumbavu wao na wema wao, na yaliyo kuwa kutokana na kukaa kwao kusikiliza kwa wizi, na kufukuzwa kwao hivi sasa. Na Aya za Sura hii zinaeleza khabari za hao wanao nyatia kwenye njia ya Uislamu na kuupinga, na ikasimulia juu ya kuisafishia misikiti kwa ajili ya kumuabudu Mwenyezi Mungu tu peke yake, na juu ya wito wa Mtume kumwendea Mwenyezi Mungu, na majini kumzunguka Mtume, na ikaeleza kwa kuwekea mipaka lipi aliwezalo Mtume na lipi ambalo haliwezi, na ikahadhirisha wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume watahadhari na Jahannamu na kubakia humo milele.
Na mwishoe Sura ikakhitimisha kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye khusika na kuijua ilimu ya ghaibu, mambo yasiyo onekana, na humdokezea anaye mteuwa katika viumbe ili awe ni Mtume wa kuuhifadhi Wahyi kwa kuulinda mpaka awafikishie  watu kwa utimilivu.  Na Mwenyezi Mungu anayajua hayo.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Sema: Imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la majini lilisikiliza, na likasema: Hakika sisi tumeisikia Qur'ani ya ajabu! Maelezo

2. Inaongoza kwenye uwongofu, kwa hivyo tumeiamini, wala hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu Mlezi. Maelezo

3. Na kwa hakika utukufu wa Mola wetu Mlezi umetukuka kabisa; hana mke wala mwana. Maelezo

4. Na kwa hakika wapumbavu miongoni mwetu walikuwa wakisema uwongo ulio pindukia mipaka juu ya Mwenyezi Mungu. Maelezo

5. Nasi tulidhani kuwa watu na majini hawamzulii uwongo Mwenyezi Mungu. Maelezo

6. Na hakika walikuwako wanaume katika watu walio kuwa wakitafuta kujikinga kwa wanaume wa kijini; kwa hivyo wakawazidisha madhambi. Maelezo

7. Na kwa hakika wao walidhani, kama mlivyo dhani nyinyi, ya kuwa Mwenyezi Mungu hatamleta Mtume. Maelezo

8. Nasi tulizigusa mbingu, na tukaziona zimejaa walinzi wenye nguvu na vimondo. Maelezo

9. Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao ili kusikiliza; lakini sasa anaye taka kusikiliza atakuta kimondo kinamvizia! Maelezo

10. Nasi hatujui kama wanatakiwa shari wale wanao kaa kwenye ardhi au Mola wao Mlezi anawatakia uwongofu. Maelezo

11. Na hakika katika sisi wamo walio wema, na wengine wetu ni kinyume na hivyo. Tumekuwa njia mbali mbali. Maelezo

12. Nasi tulijua kuwa hatutomshinda Mwenyezi Mungu duniani, wala hatuwezi kumponyoka kwa kukimbia. Maelezo

13. Nasi tulipo usikia uwongofu tuliuamini. Basi mwenye kumuamini Mola wake Mlezi basi haogopi kupunjwa wala kudhulumiwa. Maelezo

14. Na hakika wamo katika sisi Waislamu, na wamo kati yetu wanao acha haki. Basi walio silimu, hao ndio walio tafuta uwongofu. Maelezo

15. Na ama wanao acha haki, hao watakuwa kuni za Jahannamu. Maelezo

16. Na lau kama wangeli simama sawasawa juu ya njia tungeli wanywesha maji kwa wingi, Maelezo

17. Ili tuwajaribu kwa hayo. Na anaye puuza kumkumbuka Mola wake Mlezi atamsukuma kwenye adhabu ngumu. Maelezo

18. Na hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu. Maelezo

19. Na hakika Mja wa Mwenyezi Mungu alipo simama kumwomba, wao walikuwa karibu kumzonga! Maelezo

20. Sema: Hakika mimi namwomba Mola wangu Mlezi, wala simshirikishi Yeye na yeyote. Maelezo

21. Sema: Mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala kukuongozeni. Maelezo

22. Sema: Hakika hapana yeyote awezae kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitapata pa kukimbilia isipo kuwa kwake Yeye tu. Maelezo

23. Ila nifikishe Ujumbe utokao kwa Mwenyezi Mungu na risala zake. Na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika hao watapata Moto wa Jahannamu wadumu humo milele. Maelezo

24. Hata watakapo yaona wanayo ahidiwa, ndipo watakapo jua ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi. Maelezo

25. Sema: Sijui kama yapo karibu hayo mnayo ahidiwa, au Mola wangu Mlezi atayawekea muda mrefu. Maelezo

26. Yeye ndiye Mwenye kujua ya siri, wala hamdhihirishii yeyote siri yake, Maelezo

27. Isipo kuwa Mtume wake aliye mridhia. Naye huyo humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake. Maelezo

28. Ili Yeye ajue kwamba wao wamefikisha ujumbe wa Mola wao Mlezi, na Yeye anayajua vyema yote walio nayo, na amedhibiti idadi ya kila kitu. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani