Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

70. SURAT AL-MAA'RIJ

(Imeteremka Makka)

 

Katika Sura hii tukufu kipo kitisho kwa Siku ya Kiyama, na kutia khofu kwa urefu wake, na vitisho vikubwa vikubwa, na adhabu ambazo hazikubaliwi kutolewa fidia hata ya wana, wala mke, wala ndugu, wala ukoo mzima. Bali haikubaliwi fidia ya watu wa dunia nzima.
Na katika Sura hii unatolewa kombo udhaifu wa binaadamu wakati wa shida na neema, isipo kuwa aliye okolewa na Mwenyezi Mungu kwa uchamngu, na vitendo vyema. Hao wanasalimika na udhaifu huo.
Humo vile vile yanaelezwa kuchukiza tabia ya makafiri ya kuwa na tamaa ya uharibifu. Na mwishoni anausiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. awawachilie mbali na upumbavu wao na mchezo wao mpaka wakutane na siku yao waliyo ahidiwa.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayo tokea, Maelezo

2. Kwa makafiri - ambayo hapana awezaye kuizuia - Maelezo

3. Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu za daraja. Maelezo

4. Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka khamsini elfu! Maelezo

5. Basi subiri kwa subira njema. Maelezo

6. Hakika wao wanaiona iko mbali, Maelezo

7. Na Sisi tunaiona iko karibu. Maelezo

8. Siku ambayo mbingu zitakapo kuwa kama maadeni iliyo yayushwa. Maelezo

9. Na milima itakuwa kama sufi. Maelezo

10. Wala jamaa hatamuuliza jamaa yake. Maelezo

11. Ijapo kuwa wataonyeshwa waonane. Atatamani mkosefu lau ajikomboe na adhabu ya siku hiyo kwa kuwatoa fidia wanawe, Maelezo

12. Na mkewe, na nduguye, Maelezo

13. Na jamaa zake walio kuwa wakimkimu, Maelezo

14. Na wote waliomo duniani, kisha aokoke yeye. Maelezo

15. La, hasha! Kwa hakika huo ni Moto mkali kabisa, Maelezo

16. Unao babua ngozi ya kichwa! Maelezo

17. Utamwita kila aliye geuza mgongo na akageuka. Maelezo

18. Na akakusanya mali, kisha akayahifadhi. Maelezo

19. Hakika mtu ameumbwa na papara. Maelezo

20. Inapo mgusa shari hupapatika. Maelezo

21. Na inapo mgusa kheri huizuilia. Maelezo

22. Isipo kuwa wanao sali, Maelezo

23. Ambao wanadumisha Sala zao, Maelezo

24. Na ambao katika mali yao iko haki maalumu Maelezo

25. Kwa mwenye kuomba na anaye jizuilia kuomba; Maelezo

26. Na ambao wanaisadiki Siku ya Malipo, Maelezo

27. Na ambao wanaiogopa adhabu itokayo kwa Mola wao Mlezi. Maelezo

28. Hakika adhabu ya Mola wao Mlezi si ya kuaminika nayo. Maelezo

29. Na ambao wanahifadhi tupu zao. Maelezo

30. Isipo kuwa kwa wake zao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, basi hao hawalaumiwi - Maelezo

31. Lakini wanao taka kinyume ya haya, basi hao ndio wanao ruka mipaka. Maelezo

32. Na ambao wanazichunga amana zao na ahadi zao, Maelezo

33. Na ambao wanasimama imara katika ushahidi wao, Maelezo

34. Na ambao wanazihifadhi Sala zao. Maelezo

35. Hao ndio watakao hishimiwa Peponi. Maelezo

36. Wana nini wale walio kufuru wanakutumbulia macho tu? Maelezo

37. Makundi kwa makundi upande wa kulia na upande wa kushoto! Maelezo

38. Kwani kila mmoja wao anatumai kuingizwa katika Pepo ya neema? Maelezo

39. La, hasha! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na wanacho kijua. Maelezo

40. Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mashariki zote na magharibi zote kwamba Sisi tunaweza Maelezo

41. Kuwabadili kwa walio bora kuliko wao; na Sisi hatushindwi. Maelezo

42. Basi waache wapige porojo na wacheze, mpaka wakutane na siku yao wanayo ahidiwa, Maelezo

43. Siku watakapotoka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia mfundo, Maelezo

44. Macho yao yatainama, fedheha itawafunika. Hiyo ndiyo Siku waliyo kuwa wakiahidiwa. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani