Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

 

54. SURAT AL-QAMAR

(Imeteremka Makka)

 

Imekuja Aya ya kwanza katika Sura hii kuzindua kuwa watu wasikilize kwamba Kiyama kinakaribia, na watu wanahadharishwa na tukio hilo. Kisha zimekuja Aya nyengine baada yake kuweka wazi msimamo wa makafiri kwa mintarafu ya miujiza, na kushikilia kwao kukadhibisha. Na anatakiwa Mtume s.a.w. awapuuze na awangojee mpaka siku watakapo toka makaburini kama nzige walio tapanyika.
Tena baada ya hapo Aya zikawa zinafuatana, zikieleza hali namna mbali mbali za mataifa yaliyo tangulia kwa mnasaba na Mitume wao, na adhabu iliyo washukia. Na baina ya kila kisa na kingine inazindua mawazo ya kwamba Qur'ani tukufu imefanywa nyepesi kwa mwenye kutaka kuwaidhika na kuzingatia.
Mwishoe inabainisha kwamba hao makafiri wa Makka si watu wenye nguvu zaidi au wakali zaidi kushinda mataifa yaliyo kwisha tangulia, na kwamba wao si wenye kuiepuka adhabu. Tena Sura ikakhitimisha kwa kuwahadharisha wanao kadhibisha wenye inda kuwa mwisho wao watakuja tumbukizwa Motoni kifudifudi, na wataambiwa: Onjeni mguso wa Jahannamu mliyo kuwa mkiikadhibisha. Na inawatuza wachamngu katika maskani zao za Mabustanini na mito, katika makao mazuri kwa Mfalme Mwenye uweza.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Saa imekaribia, na mwezi umepasuka! Maelezo 

2. Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: Huu uchawi tu unazidi kuendelea. Maelezo 

3. Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao. Na kila jambo ni lenye kuthibiti. Maelezo 

4. Na bila ya shaka zimewajia khabari zenye makaripio. Maelezo 

5. Hikima kaamili; lakini maonyo hayafai kitu! Maelezo 

6. Basi jiepushe nao. Siku atakapo ita mwitaji kuliendea jambo linalo chusha; Maelezo 

7. Macho yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige walio tawanyika, Maelezo 

8. Wanamkimbilia mwitaji, na makafiri wanasema: Hii ni siku ngumu. Maelezo 

9. Kabla yao kaumu ya Nuhu walikanusha; wakamkanusha mja wetu, na wakasema ni mwendawazimu, na akakaripiwa. Maelezo 

10. Basi akamwomba Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru! Maelezo 

11. Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayo miminika. Maelezo 

12. Na tukazipasua ardhi kwa chemchem, yakakutana maji kwa jambo lilio kadiriwa. Maelezo 

13. Na tukamchukua kwenye safina ya mbao na kamba. Maelezo 

14.Ikawa inakwenda kwa nadhari yetu, kuwa ni malipo kwa alivyo kuwa amekanushwa. Maelezo 

15. Na bila ya shaka tuliiacha iwe ni Ishara. Lakini je, yupo anaye kumbuka? Maelezo 

16. Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo yangu. Maelezo 

17. Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anaye kumbuka? Maelezo 

18. Kina A'di walikanusha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu? Maelezo 

19. Hakika Sisi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku korofi mfululizo, Maelezo 

20. Ukiwang'oa watu kama vigogo vya mitende vilio ng'olewa. Maelezo 

21. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu? Maelezo 

22. Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani nyepesi kufahamika; lakini yupo anaye kumbuka? Maelezo 

23. Thamudi waliwakanusha Waonyaji. Maelezo 

24. Wakasema: Ati tumfuate binaadamu mmoja katika sisi? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotofu na kichaa! Maelezo 

25. Ni yeye tu aliye teremshiwa huo ukumbusho kati yetu sote? Bali huyu ni mwongo mwenye kiburi! Maelezo 

26. Kesho watajua ni nani huyo mwongo mwenye kiburi. Maelezo 

27. Hakika Sisi tutawapelekea ngamia jike ili kuwajaribu, basi watazame tu na ustahamili. Maelezo 

28. Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu ya maji itahudhuriwa na aliye khusika. Maelezo 

29. Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja. Maelezo 

30. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu! Maelezo 

31. Hakika Sisi tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama mabuwa ya kujengea uwa. Maelezo 

32. Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kwa kukumbuka, lakini yupo akumbukaye? Maelezo 

33. Kaumu Lut'i nao waliwakadhibisha Waonyaji. Maelezo 

34. Hakika Sisi tukawapelekea kimbunga cha vijiwe, isipo kuwa wafuasi wa Lut'i. Hao tuliwaokoa karibu na alfajiri. Maelezo 

35. Kwa neema inayo toka kwetu. Hivyo ndivyo tumlipavyo anaye shukuru. Maelezo 

36. Na hakika yeye aliwaonya adhabu yetu; lakini wao waliyatilia shaka hayo maonyo. Maelezo 

37. Na walimtaka awape wageni wake. Tukayapofua macho yao, na tukawaambia: Onjeni basi adhabu na maonyo yangu! Maelezo 

38. Na iliwafikia wakati wa asubuhi adhabu yangu ya kuendelea. Maelezo 

39. Basi onjeni adhabu na maonyo yangu! Maelezo 

40. Na hakika tumeisahilisha Qur'ani kuikumbuka. Lakini yupo anaye kumbuka? Maelezo 

41. Na Waonyaji waliwafikia watu wa Firauni. Maelezo 

42. Walizikadhibisha Ishara zetu zote, nasi tukawashika kama anavyo shika Mwenye nguvu Mwenye uweza. Maelezo 

43. Je! Makafiri wenu ni bora kuliko hao, au yameandikwa vitabuni kuwa nyinyi hamtiwi makosani? Maelezo 

44. Au ndio wanasema: Sisi ni wengi tutashinda tu. Maelezo 

45. Wingi wao huu utashindwa, na wao watasukumwa nyuma. Maelezo 

46. Bali Saa ya Kiyama ndio miadi yao, na Saa hiyo ni nzito zaidi na chungu zaidi. Maelezo 

47. Hakika wakosefu wamo katika upotofu na wazimu. Maelezo 

48. Siku watakapo kokotwa Motoni kifudifudi waambiwe: Onjeni mguso wa Jahannamu! Maelezo 

49. Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo. Maelezo

50. Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho. Maelezo 

51. Na bila ya shaka tumekwisha waangamiza wenzenu. Lakini yupo anaye kumbuka? Maelezo

52. Na kila jambo walilo lifanya limo vitabuni. Maelezo

53. Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa. Maelezo

54. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na mito. Maelezo

55. Katika makalio ya haki kwa Mfalme Mwenye uweza. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani