Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

41. SURAT FUSS'ILAT (AU H'A MIM SAJDAH)

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii imeanzia kwa harufi mbili katika harufi za alifbete kama inavyo fanya Qur'ani katika Sura nyingi. Sura hii imeeleza katika nyingi ya Aya zake shani ya Qur'ani na mambo iliyo kusanya yaliyo khusu bishara na maonyo. Na imeeleza msimamo wa washirikina kukhusu Qur'ani, katika kuipuuza na kuupiga vita wito wake, na msimamo wa Mtume kwa mnasaba wa makafiri, kwa kusimama imara juu ya wito wake kwao na kuwaambia: "Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; inafunuliwa kwangu ya kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Basi tengeneeni kumwendea Yeye, na mumtake msamaha." Na Sura inaingilia kuwakumbusha washirikina uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kuziumba mbingu na ardhi, kisha inawahadharisha na yaliyo watokelea watu wa mataifa walio karibu mno na makwao, nao ni kina A'adi na Thamudi. Na inawakumbusha Siku ya Akhera, siku yatakapo washuhudia masikio yao, na macho yao, na ngozi zao, kwa waliyo kuwa wakiyatenda; na mijadiliano itakayo kuwa baina yao na viungo vyao siku hiyo; na watayo  yaomba wafwasi kwa Mola wao Mlezi Siku ya Kiyama: "Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe wale walio tupoteza miongoni mwa majini na watu ili tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni mwa walio chini kabisa." Na kama ilivyo kuwa mwendo wa Mwenyezi Mungu katika Kitabu hichi akisimulia khabari ya makafiri, husimulia pia khabari za Waumini. Basi Sura hii  imesimulia khabari za walio sema: "Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu", kisha wakasimama sawa sawa, neema za daima alizo waneemesha, na akalinganisha baina ya kheri na shari: "Wema haulingani na uovu".
Kisha Sura inataka watu waangalie Ishara za uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu zinazo onyesha kumkinika kufufuliwa maiti, kisha inarejea tena kuzidi kuwakemea wanao zigeuza Aya za Mwenyezi Mungu, na kwamba hao hawamkhofu Mwenyezi Mungu. Na kwamba hakika Kitabu hichi hakiingiliwi na upotovu kutoka mbele yake wala nyuma yake. Huu ni mteremsho ulio tokana na Mwenye hikima, Msifika. Na hakika Ujumbe wa Muhammad si ujumbe ulio zuliwa tu.
Na Sura inathibitisha khulka moja katika khulka za binaadammu, nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu akimneemesha mtu huipuuza Haki, na ikimgusa tu shari anakuwa na madua marefu marefu.
Na Sura imekhitimisha kwa kuthibitisha mambo mawili muhimu kabisa, nayo ni la kwanza: kutaja kwa Qur'ani Tukufu yenyewe Haki iliyomo ndani yake isiyo na shaka yoyote: "Tutawaonyesha Aya zetu katika upeo wa macho na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli."  Na la pili lake kuwa hilo wanalo litegemea makafiri si lolote  ila ni shaka tu ya kufufuliwa iliyo wapelekea kuwa nayo ukafiri na upotovu. "Ama hakika wao bado wamo katika shaka ya kukutana na Mola wao Mlezi. Hakika Yeye amekizunguka kila kitu."


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. H'a Mim Maelezo

2. Uteremsho huu umetoka kwa Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Maelezo

3. Hichi ni Kitabu kilicho pambanuliwa Aya zake, cha kusomwa kwa Kiarabu kwa watu wanao jua. Maelezo

4. Kitoacho khabari njema, na chenye kuonya. Lakini wengi katika wao wamepuuza; kwa hivyo hawasikii. Maelezo

5. Na wakasema: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa hayo unayo tuitia, na masikio yetu yana uziwi, na baina yetu na wewe lipo pazia. Basi wewe tenda, nasi tunatenda. Maelezo

6. Sema: Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; inafunuliwa kwangu ya kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Basi nyookeni sawa kumwendea Yeye, na mumtake msamaha, na ole wao wanao mshirikisha, Maelezo

7. Ambao hawatoi Zaka na wanaikataa Akhera. Maelezo

8. Hakika wanao amini na wakatenda mema watakuwa na ujira usio na ukomo. Maelezo

9. Sema: Hivyo nyinyi mnamkataa aliye umba ardhi katika siku mbili, na mnamfanyia washirika? Huyu ndiye Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

10. Na akaweka humo milima juu yake, na akabarikia humo na akakadiria humo chakula chake katika siku nne. Haya ni sawa kabisa kwa wanao uliza. Maelezo

11. Kisha akazielekea mbingu, na zilikuwa moshi, akaziambia hizo na ardhi: Njooni, kwa khiari au kwa nguvu! Vyote viwili vikasema: Tumekuja nasi ni wat'iifu. Maelezo

12. Basi akazifanya mbingu saba kwa siku mbili, na akazipangia kila mbingu mambo yake. Na tukaipamba mbingu ya chini kwa mataa na kwa ulinzi. Hichi ndicho kipimo cha Mwenyezi Mungu Mwenye Kujua. Maelezo

13. Basi wakipuuza wewe sema: Nakuhadharisheni adhabu mfano wa adhabu ya A'di na Thamudi, Maelezo

14. Walipo wajia Mitume mbele yao na nyuma yao wakawaambia: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu! Wakasema: Angeli taka Mola wetu Mlezi bila ya shaka angeli wateremsha Malaika. Basi sisi hakika tunayakataa hayo mliyo tumwa. Maelezo

15. Ama kina A'di walijivuna katika nchi bila ya haki, na wakasema: Nani aliye kuwa na nguvu kushinda sisi? Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu aliye waumba ni Mwenye nguvu kushinda wao? Na wao wakawa wanazikataa Ishara zetu! Maelezo

16. Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku za ukorofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katika uhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu ya Akhera ina hizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa. Maelezo

17. Na ama Thamudi tuliwaongoza, lakini walipenda upofu kuliko uwongofu. Basi uliwachukua moto wa adhabu ya kuwafedhehi kwa sababu ya yale waliyo kuwa wakiyachuma. Maelezo

18. Na tukawaokoa walio amini na wakawa wanamcha-mngu. Maelezo

19. Na siku watakapo kusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu kwenye Moto, nao wakikgawanywa kwa makundi. Maelezo

20. Hata watakapo ufikia Moto yatawashuhudia masikio yao, na macho yao na ngozi zao kwa waliyo kuwa wakiyatenda. Maelezo

21. Na wao wataziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia? Nazo zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu ambaye ametamkisha kila kitu! Na Yeye ndiye aliye kuumbeni mara ya kwanza, na kwake Yeye tu mtarejeshwa. Maelezo

22. Na hamkuwa wenye kujificha hata masikio yenu, na macho yenu, na ngozi zenu, zisikushuhudilieni. Lakini mlidhani kwamba Mwenyezi Mungu hayajui mengi katika mliyo kuwa mkiyatenda. Maelezo

23. Basi hiyo dhana yenu mliyo kuwa mkimdhania Mola wenu Mlezi. Imekuangamizeni; na mmekuwa miongoni mwa walio khasiri. Maelezo

24. Basi wakisubiri Moto ndio maskani yao. Na wakiomba radhi hawakubaliwi. Maelezo

25. Na tukawawekea marafiki, na wakawapambia yaliyo mbele yao na nyuma yao. Basi ikawathibitikia kauli wawe pamoja na mataifa yaliyo pita kabla yao, miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa ni wenye kukhasirika. Maelezo

26. Na walio kufuru walisema: Msiisikilize Qur'ani hii, na timueni zogo, huenda mkashinda. Maelezo

27. Basi hapana shaka tutawaonjesha hao walio kufuru adhabu kali, na hapana shaka tutawalipa malipo mabaya ya yale waliyo kuwa wakiyafanya. Maelezo

28. Hayo ndiyo malipo ya Maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto! Humo watakuwa na maskani ya kudumu, ndiyo malipo yao kwa sababu walikuwa wakizikataa Ishara zetu. Maelezo

29. Na walio kufuru watasema: Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe walio tupoteza miongoni mwa majini na watu ili tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni wa walio chini kabisa. Maelezo

30. Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa. Maelezo

31. Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na katika Akhera, na humo mtapata kinacho tamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyo vitaka. Maelezo

32. Ni takrima itokayo kwa Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Maelezo

33. Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu? Maelezo

34. Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu. Maelezo

35. Lakini hawapewi wema huu ila wanao subiri, wala hawapewi ila wenye bahati kubwa. Maelezo

36. Na Shet'ani akikuchochea kwa uchochezi wewe jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. Maelezo

37. Na katika Ishara zake ni usiku na mchana, na jua na mwezi. Basi msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliye viumba, ikiwa nyinyi mnamuabudu Yeye tu. Maelezo

38. Na ikiwa watajivuna, basi hao walioko kwa Mola wako Mlezi wanamtakasa Yeye usiku na mchana, na wao hawachoki. Maelezo

39. Na katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi nyonge, lakini tunapo iteremshia maji mara unaiona inataharaki na kuumuka. Bila ya shaka aliye ihuisha ardhi ndiye atakaye huisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu. Maelezo

40. Hakika wale wanao upotoa ukweli uliomo katika Ishara zetu hawatufichikii Sisi. Je! Atakaye tupwa Motoni ni bora au atakaye kuja kwa amani Siku ya Kiyama? Tendeni mpendavyo, kwa hakika Yeye anayaona mnayo yatenda. Maelezo

41. Kwa hakika wanayo yakataa mawaidha haya yanapo wajia (wataangamia), na haya bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu. Maelezo

42. Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake. Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa. Maelezo

43. Huambiwi ila yale yale waliyo ambiwa Mitume wa kabla yako. Hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ni Mwenye maghfira, na ni Mwenye adhabu chungu. Maelezo

44. Na lau tungeli ifanya Qur'ani kwa lugha ya kigeni wangeli sema: Kwanini Aya zake haziku pambanuliwa? Yawaje lugha ya kigeni na Mtume Mwaarabu? Sema: Hii Qur'ani ni uwongofu na poza kwa wenye kuamini. Na wasio amini umo uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. Hao wanaitwa nao wako pahala mbali. Maelezo

45. Na hakika tulimpa Musa Kitabu, lakini pakatokea khitilafu kati yake. Na lau kuwa halikwisha tangulia neno la Mola wako Mlezi wangeli hukumiwa. Na hakika wao wamo katika shaka yenye kuwatia wasiwasi. Maelezo

46. Anaye tenda mema basi anajitendea mwenyewe nafsi yake, na mwenye kutenda uovu basi ni juu ya nafsi yake vile vile; wala Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja. Maelezo

47. UJUZI wa kuijua Saa ya Kiyama unarudishwa kwake tu Mwenyezi Mungu. Na matunda hayatoki katika mafumba yake, wala mwanamke hachukui mimba, wala hazai, ila kwa kujua kwake. Na siku atakayo waita, akawaambia: Wako wapi washirika wangu? Hapo watasema: Tunakiri kwako ya kwamba hapana miongoni mwetu anaye shuhudia hayo. Maelezo

48. Na wakawapotea wale walio kuwa wakiwaomba hapo kwanza, na wakawa na yakini kuwa hawana pa kukimbilia. Maelezo

49. Mwanaadamu hachoki kuomba dua za kheri, na inapo mpata shari, mara huvunjika moyo akakata tamaa. Maelezo

50. Na pindi tukimwonjesha rehema itokayo kwetu baada ya kumgusa dhara, bila ya shaka husema: Haya nayastahiki mimi, wala sidhani kuwa Kiyama kitakuja. Na hata nikirudishwa kwa Mola wangu Mlezi bila ya shaka nina mema yangu kwake! Basi kwa yakini tutawaelezea walio kufuru hayo waliyo yatenda, na kwa yakini tutawaonjesha adhabu ngumu. Maelezo

51. Na tukimneemesha mwanaadamu hugeuka na kujitenga upande, na inapo mgusa shari, huwa na madua marefu marefu. Maelezo

52. Sema: Mnaonaje! Ikiwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi ikawa ndio mmeyakataa, ni nani aliye potea zaidi kuliko aliye katika upinzani wa mbali? Maelezo

53. Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu? Maelezo

54. Ama wao wamo katika shaka ya kukutana na Mola wao Mlezi! Ama hakika Yeye amekizunguka kila kitu. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani