Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani√‚¬  (Nani Yeye?)

 

36. SURAT YA-SIN

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii imeanzia kwa harufi mbili ambazo ni katika harufi za kuundiwa maneno ya Kiarabu. Na ikafuatiliza kwa kuapa kwa Qur'ani ya kwamba Muhammad s.a.w. bila ya shaka ni miongoni mwa Mitume, walio tumwa. Na kuwa hakika yeye yuko kwenye Njia Iliyo Nyooka iliyo rasimiwa na Qur'ani aliyo teremshiwa yeye kutokana na Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu, ili apate kuwaonya kwayo watu ambao baba zao hawakupata kabla yake kuonywa. Tena Sura ikaingia kutufanyia taswira, picha,√‚¬  ya wanao kataa, ambao hawanafiiki na maonyo. Na inatubainishia kwamba kuonya humfaidisha mwenye kuelekea kupokea makumbusho, na kumcha Mwingi wa Rehema. Na kwamba hakika Mwenyezi Mungu atawafufua wafu, na atavihisabu vitendo vya waja. Na Sura ikaingilia kuwapigia mfano makafiri wa Makka, na ikabainisha mvutano baina ya wanao mlingania Mwenyezi Mungu na wanao kadhibisha. Inabainisha mwisho wa makundi mawili hayo. Kisha ikawa inaeleza dalili za uweza unao pasa kuuamini na kuogopa miadi ya Mwenyezi Mungu itakayo watokea ghafla katika Siku ambayo kila mtu atalipwa kwa aliyo yatenda. Watu wa Peponi watastareheshwa. Watapata wanacho kitamani. Na watu wa Motoni watafukuzwa. Nao watakuwa katika mbano wa uweza wa Mwenyezi Mungu. Midomo yao itazibwa, na viungo vyao ndivyo vitavyo tamka. Na Mwenyezi Mungu angeli penda, basi bila ya shaka angeli zigeuza sura zao pia. Kwani ni Yeye ndiye Mwenye kumbadilisha anaye mrefushia umri wake duniani badala ya nguvu akawa dhaifu, na badala ya akili akawa amepiswa. Na Yeye ndiye aliye mlinda Nabii wake na kuzugwa na kichaa. Naye hakumfundisha utungaji mashairi, na wala hauhitajiki ufundi huo unao mfanya aliye nao kutanga tanga katika kila bonde. Mtume hakuja ila kwa ajili ya ukumbusho ulio wazi, ulio tokana na akili, sio ulio tokana na mawazo mapepe tu.√‚¬  Na Sura ikaendelea kukumbusha fadhila za Mwenyezi Mungu juu ya waja wake, na kwamba Yeye amewafanya wanyama wa mifugo ambao wanawamiliki na wanawapanda wawatumikie. Na juu ya neema hizi zilio wekwa kwa faida yao, wao bado wanakwenda kuabudu miungu ya ushirikina isiyo weza kitu. Na Sura inakhitimisha kwa kumtaka binaadamu aangalie namna alivyo umbwa kutokana na tone la manii, na khalafu yeye anakuwa ni mpinzani wa kudhihirisha upinzani wake. Na yule aliye umba hapo mwanzo, na anaye toa moto kutoka mti wa kijani, na aliye umba mbingu na ardhi, huyo basi ni Muweza wa kuyafufua mafupa nayo yamekwisha vurugika. Na amri yake ni kukiambia kitu: Kuwa! Na kikawa. Ametakasika Mwenye kumiliki kila kitu. Na kwake Yeye mtarejea.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Ya-Sin (Y.S.). Maelezo

2. Kwa Haki ya Qur'ani yenye hikima! Maelezo

3. Hakika wewe ni miongoni mwa walio tumwa, Maelezo

4. Juu ya Njia Iliyo Nyooka. Maelezo

5. Uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. Maelezo

6. Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa , basi wao wamekuwa wenye kughafilika. Maelezo

7. Bila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao, kwa hivyo hawaamini. Maelezo

8. Tumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo vichwa vyao viko juu tu. Maelezo

9. Tumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao, na tumewafunika macho yao; kwa hivyo hawaoni. Maelezo

10. Ni sawa sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini. Maelezo

11. Hakika wewe unamwonya mwenye kufuata ukumbusho, na akamcha Arrahman, Mwingi wa Rehema, kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo msamaha na ujira mwema. Maelezo

12. Hakika Sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayo yatanguliza, na wanayo yaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asli lenye kubainisha. Maelezo

13. Na wapigie mfano wa wakaazi wa mji walipo wafikia walio tumwa. Maelezo

14. Tulipo watumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawazidishia nguvu kwa mwingine wa tatu. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu. Maelezo

15. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na Mwingi wa Rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu. Maelezo

16. Wakasema: Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa kwenu. Maelezo

17. Wala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi. Maelezo

18. Wakasema: Sisi tumeagua kuwa nyinyi ni wakorofi. Ikiwa hamtaacha basi kwa yakini tutakupigeni mawe, na mtapata adhabu chungu kutoka kwetu. Maelezo

19. Wakasema: Ukorofi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa? Ama nyinyi ni watu walio pindukia mipaka. Maelezo

20. Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa. Maelezo

21. Wafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe wameongoka. Maelezo

22. NA KWA NINI nisimuabudu yule aliye niumba na kwake mtarejeshwa? Maelezo

23. Je! Niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani, Mwingi wa Rehema, akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa. Maelezo

24. Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio dhaahiri. Maelezo

25. Hakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni! Maelezo

26. Akaambiwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti kuwa watu wangu wangeli jua Maelezo

27. Jinsi Mola wangu Mlezi alivyo nisamehe, na akanifanya miongoni mwa walio hishimiwa. Maelezo

28. Na hatukuwateremshia kaumu yake baada yake jeshi kutoka mbinguni, wala si wenye kuteremsha. Maelezo

29. Hakukuwa ila ukelele mmoja tu; na mara walizimwa! Maelezo

30. Nawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wao humkejeli. Maelezo

31. Je! Hawaoni umma ngapi tulizo ziangamiza kabla yao? Hakika hao hawarejei tena kwao. Maelezo

32. Na hapana mmoja ila wote watakusanywa waletwe mbele yetu. Maelezo

33. Na Ishara hiyo kwao - ardhi iliyo kufa, nasi tukaifufua, na tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanazila! Maelezo

34. Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na tukatimbua chemchem ndani yake, Maelezo

35. Ili wale matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikono yao! Basi je, hawashukuru? Maelezo

36. Subhana, Ametakasika, aliye umba dume na jike vyote katika vinavyo mea katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyo vijua. Maelezo

37. Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa gizani. Maelezo

38. Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua. Maelezo

39. Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe. Maelezo

40. Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea katika njia zao. Maelezo

41. Na ni Ishara kwao kwamba Sisi tuliwapakia dhuriya zao katika jahazi ilio sheheni. Maelezo

42. Na tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyo vipanda. Maelezo

43. Na tukitaka tunawazamisha, wala hapana wa kuwasaidia, wala hawaokolewi, Maelezo

44. Isipo kuwa kwa rehema zitokazo kwetu na starehe kwa muda. Maelezo

45. Na wanapo ambiwa: Jilindeni na yalioko mbele yenu na yalioko nyuma yenu, ili mpate kurehemewa... Maelezo

46. Na haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa ni wenye kuipuuza. Maelezo

47. Na wanapo ambiwa: Toeni katika aliyo kupeni Mwenyezi Mungu, walio kufuru huwaambia walio amini: Je! Tuwalishe ambao Mwenyezi Mungu angependa angeli walisha mwenyewe? Nyinyi hammo ila katika upotofu ulio dhaahiri. Maelezo

48. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli? Maelezo

49. Hawangojei ila ukelele mmoja tu utakao wachukua nao wamo kuzozana. Maelezo

50. Basi hawataweza kuusia, wala kwa watu wao hawarejei. Maelezo

51. Na litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao Mlezi. Maelezo

52. Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume. Maelezo

53. Haitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhuruishwa mbele yetu. Maelezo

54. Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale mliyo kuwa mkiyatenda. Maelezo

55. Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi. Maelezo

56. Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fakhari. Maelezo

57. Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakacho kitaka. Maelezo

58. "Salama!" Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu. Maelezo

59. Na enyi wakosefu! Jitengeni leo! Maelezo

60. Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet'ani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu. Maelezo

61. Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. Maelezo

62. Na bila ya shaka yeye amekwisha lipoteza kundi kubwa miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkifikiri? Maelezo

63. Hii basi ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa. Maelezo

64. Ingieni leo kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru. Maelezo

65. Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma. Maelezo

66. Na tungeli penda tungeli yafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wange ionaje? Maelezo

67. Na tungeli taka tunge wageuza sura hapo hapo walipo, basi wasinge weza kwenda wala kurudi. Maelezo

68. Na tunaye mzeesha tunamrudisha nyuma katika umbo. Basi je! hawazingatii? Maelezo

69. Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur'ani inayo bainisha. Maelezo

70. Ili imwonye aliye hai, na neno litimie juu ya makafiri. Maelezo

71. Je! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyo fanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki. Maelezo

72. Na Sisi tukawadhalilishia. Basi baadhi yao wako wanao wapanda, na baadhi yao wanawala. Maelezo

73. Na wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru? Maelezo

74. Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati wapate kusaidiwa! Maelezo

75. Hawataweza kuwasaidia. Bali hao ndio watakuwa askari wao watakao hudhurishwa. Maelezo

76. Basi maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika Sisi tunayajua wanayo yaweka siri na wanayo yatangaza. Maelezo

77. Kwani mwanaadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana na tone la manii? Kisha sasa yeye ndio amekuwa ndiye mgomvi wa dhaahiri! Maelezo

78. Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung'unyika? Maelezo

79. Sema: Ataihuisha huyo huyo aliye iumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba. Maelezo

80. Aliye kujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa kwa huo mnawasha. Maelezo

81. Kwani aliye ziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi. Maelezo

82. Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa. Maelezo

83. Basi Ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake Yeye mtarejeshwa. Maelezo √‚¬  √‚¬ 


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright √‚¬© 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani