Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

 

31. SURAT LUQMAN

(Imeteremka Makka)

 

Imeanza Sura hii tukufu kwa kueleza khabari za hichi Kitabu na uwongofu na rehema ziliomo ndani yake. Na wamesifiwa watu wema kwa kuwa wana ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu, na wanaiamini Akhera, na watapata mafanikio. Na kinyume cha hayo yametajwa ya walio potea, wenye kiburi. Na wamebashiriwa Waumini kuwa watapata malipo mazuri katika makaazi ya Peponi. Na macho yanatakiwa yaangalie Ishara za ulimwengu zinazo onyesha uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Upweke wake. Na Sura hii inawakabili makafiri kwa kuwaambia kwamba kwa hakika Mwenyezi Mungu wanaye muwekea washirika ameumba asicho kiweza yeyote asiye kuwa Yeye kukiumba. Tena Sura ikaingia kutaja wasia wa Luqman kumuusia mwanawe mausio yaliyo changanyika na mausio ya mtu na wazazi wake. Na ikaeleza mambo aliyo yat'iisha Mwenyezi Mungu kwa faida ya mwanaadamu, na neema zinazo onekana na zisio onekana alizo mjazia mwanaadamu.
Na ikaeleza khabari za wanao jadili mambo yaliyo mkhusu Mwenyezi Mungu bila ya ujuzi, na wanao toa udhuru kwa upotovu wao kuwa wanawafuata waliyo kuwa wakiyafuata baba zao. Na Sura ikamsifu anaye uelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu naye akawa ni mtenda mema, na ikamnasihi Mtume asihuzunike kwa kukataa kwa mwenye kukufuru, kwani marejeo ya huyo ni kwa Mwenyezi Mungu. Na ikafafanua kwa wingi mambo yanayo onyesha uweza, na utukufu, na rehema.
Na Sura imeamrisha kumcha Mwenyezi Mungu, na kuogopa hisabu na malipo. Na imehadharisha ghururi,  kudanganyika, na kumt'ii Shet'ani. Na ikakhitimisha kwa kutaja kuwa Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye ujuzi kamili wa kila kitu. Na muhimu ya iliyo kusanya Sura hii ni mambo matatu:

·        Kwanza: Kuwabashiria watu wema kuwa watapata neema na furaha, na kuwaonya makafiri kuwa watapata adhabu.

·       Pili: Kueleza Ishara za ulimwengu na mambo yaliyo wazi yenye kuonyesha uweza wa Mwenyezi Mungu, na Upweke wake, na upeo wa utukufu wake na rehema yake.

·       Tatu: Wasia mkuu ulio kusudiwa usalama wa itikadi, na kulinda ut'iifu na tabia njema.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Alif Lam Mim (A.L.M.) Maelezo

2. Hizi ni Aya za Kitabu chenye hikima. Maelezo

3. Kuwa ni Uwongofu na Rehema kwa wafanyao wema, Maelezo

4. Wanao shika Sala, na wanatoa Zaka, nao wana yakini na Akhera. Maelezo

5. Hao ndio walio na uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio wenye kufanikiwa. Maelezo

6. Na miongoni mwa watu wapo wanao nunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha. Maelezo

7. Na (mtu kama huyo) anapo somewa Aya zetu huzipa mgongo kwa kujivuna, kama kwamba hakuzisikia, kama kwamba masikioni mwake mna uziwi. Basi mbashirie kuwa atapata adhabu chungu. Maelezo

8. Hakika walio amini na wakatenda mema watakuwa nazo Bustani za neema. Maelezo

 

9. Watadumu humo - ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kweli. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. Maelezo

10. Ameziumba mbingu bila ya nguzo mnazo ziona; na ameweka katika ardhi milima ili ardhi isikuyumbisheni; na ametawanya humo kila namna ya wanyama; na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha katika ardhi mimea mizuri ya kila namna. Maelezo

11. Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni wameumba nini hao wasio kuwa Yeye! Lakini madhaalimu wamo katika upotovu uliyo dhaahiri. Maelezo

12. Na tulimpa Luqman hikima, tukamwambia: Mshukuru Mwenyezi Mungu. Na mwenye kushukuru basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na aliye kufuru, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Msifiwa. Maelezo

13. Na Luqman alipo mwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu. Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhulma iliyo kubwa. Maelezo

14. Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio. Maelezo

15. Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwat'ii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya anaye elekea kwangu. Kisha marejeo yenu ni kwangu Mimi, na Mimi nitakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda. Maelezo

16. Ewe mwanangu! Kikiwapo kitu cha uzito wa chembe ya khardali kikawa ndani ya jabali au ndani ya mbingu au ndani ya ardhi, basi Mwenyezi Mungu atakileta. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika, Mwenye khabari za yote. Maelezo

17. Ewe mwanangu! Shika Sala, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayo kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.. Maelezo

18. Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna na kujifakhirisha. Maelezo

19. Na ushike mwendo wa katikati, na teremsha sauti yako. Hakika katika sauti mbaya zote bila ya shaka iliyo zidi ni sauti ya punda. Maelezo

20. Kwani hamwoni ya kwamba Mwenyezi Mungu amevifanya vikutumikieni viliomo mbinguni na kwenye ardhi, na akakujalizieni neema zake, za dhaahiri na za siri? Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu pasipo ilimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru. Maelezo

21. Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, husema: Bali tunafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je! Ijapo kuwa Shet'ani anawaita kwenye adhabu ya Moto uwakao? Maelezo

22. Na mwenye kuuelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa anafanya wema, basi huyo hakika amekwisha kamata fundo lilio madhubuti. Na mwisho wa mambo yote ni kwa Mwenyezi Mungu. Maelezo

23. Na anaye kufuru, isikuhuzunishe kufuru yake. Kwetu ndio marudio yao, na hapo tutawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani. Maelezo

24. Tunawastarehesha kwa uchache, kisha tutawasukuma kwenye adhabu ngumu. Maelezo

25. Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Wewe sema: Alhamdulillahi! Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui. Maelezo

26. Ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni na katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mkwasi, Mwenye kusifiwa. Maelezo

27. Na lau kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni kalamu, na bahari (ikawa wino), na ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingeli kwisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. Maelezo

28. Hakukuwa kuumbwa kwenu, wala kufufuliwa kwenu ila ni kama nafsi moja tu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona. Maelezo

29. Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu huuingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku, na amedhalilisha jua na mwezi? Vyote hivyo vinakwenda mpaka wakati ulio wekwa. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda. Maelezo

30. Hivi ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye wa kweli, na hakika wanacho kiomba ni cha uwongo. Na kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mtukufu na ndiye Mkubwa. Maelezo

31. Kwani huoni kwamba marikebu hupita baharini zikichukua neema za Mwenyezi Mungu, ili kukuonyesheni baadhi ya Ishara zake? Hakika katika haya zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri, mwenye kushukuru. Maelezo

32. Na wimbi linapo wafunika kama wingu, wao humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia dini. Lakini anapo waokoa wakafika nchi kavu, wapo baadhi yao huenda mwendo wa sawa. Wala hazikanushi Ishara zetu ila aliye khaini kafiri mkubwa. Maelezo

33. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi, na iogopeni siku ambayo mzazi hatamfaa mwana, wala mwana hatamfaa mzazi kwa lolote. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala asikudanganyeni na Mwenyezi Mungu mdanganyifu. Maelezo

34. Hakika kuijua Saa (ya Kiyama) kuko kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye ndiye anaye iteremsha mvua. Na anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani