Sura hii ya Makka imeteremka Makka, na ina Aya 109. Imeanzia kuashiria
cheo cha Kitabu hiki Kitukufu, na wasemayo washirikina yaliyo mkhusu Nabii
s.a.w. Kisha ikataja ulimwengu na ishara za Mwenyezi Mungu Mtukufu ziliomo
humo, na malipo ya Siku ya Kiyama, na mwendo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu
kuwatendea makafiri, na kuwakemea kwake kwa hizo itikadi zao, na hali ya
watu wakati wa shida na neema, na uwezo wa Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu,
na kuemewa masanamu kufanya lolote. Na katika Sura hii wanatakiwa
kama wanaweza makafiri walete Sura japo moja ya kuzua. Na pia ndani yake
kuna vitisho vikali vya adhabu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na hali za nafsi
za watu, na vipi Mwenyezi Mungu anavyo vichunguza vitendo vyao. Kisha baada
ya hayo ikaingia kumwondolea Nabii s.a.w. kuungulika kwake kwa ukafiri
wao, pamoja na kutoa hoja ya kuwavunja kabisa, na ikampoza kwa kumtajia
hadithi za Manabii wengine na kaumu zao. Ikaja hadithi ya Nuhu, na hadithi
ya Musa na Harun na Firauni na Wana wa Israili; kisha ikaashiriwa hadithi
ya Yunus, na kwa jina hilo Sura hii ikaitwa. Na mwisho ikaelekea
Sura hii kubainisha mambo ya Mtume huyu ili kutimiza mawaidha na mazingatio.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Alif Lam Ra. Hizo ni Aya za Kitabu chenye Hikima.
***
2. Je! Imekuwa ajabu kwa watu kwamba tumemfunulia
mmoja wao kuwa: Waonye watu, na wabashirie wale walio amini ya kuwa watakuwa
na cheo cha juu kwa Mola wao Mlezi? Wakasema makafiri: Hakika huyu ni mchawi
dhaahiri!
***
3. Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi Mungu, ambaye
ameziumba mbingu na ardhi kwa siku sita, na ametawala kwenye ufalme wake,
anaendesha mambo yote. Hapana mwombezi ila baada ya idhini yake. Huyo ndiye
Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Je! Hamkumbuki?
***
4. Kwake Yeye tu ndio marejeo yenu nyote. Hii
ni ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo ya kweli. Hakika Yeye ndiye aliye anzisha
uumbaji, na kisha ataurejesha ili awalipe kwa uadilifu wale walio amini
na wakatenda mema. Na walio kufuru, wao watapata vinywaji vinavyo chemka,
na adhabu chungu kwa sababu ya walivyo kuwa wakikufuru.
***
5. Yeye ndiye aliye lijaalia jua kuwa na mwangaza,
na mwezi ukawa na nuru, na akaupimia vituo ili mjue idadi ya miaka na hisabu.
Mwenyezi Mungu hakuviumba hivyo ila kwa Haki. Anazipambanua Ishara kwa
watu wanao jua.
***
6. Hakika katika kukhitalifiana usiku na mchana,
na katika alivyo umba Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi, zipo Ishara
kwa watu wanao mcha-Mngu.
***
7. Hakika wasio taraji kukutana nasi, na wakaridhia
maisha ya dunia na wakatua nayo, na walio ghafilika na Ishara zetu,
***
8. Hao, makaazi yao ni Motoni kwa sababu ya waliyo
kuwa wakiyachuma.
***
9. Hakika walio amini na wakatenda mema, Mola
wao Mlezi atawaongoa kwa sababu ya Imani yao. Itakuwa inapita mito kati
yao katika Mabustani yenye neema.
***
10. Wito wao humo utakuwa: Subhanaka Llahumma
"Umetakasika Ee Mwenyezi Mungu!" Na maamkio yao humo ni "Salama". Na mwisho
wa wito wao ni: Alhamdulillahi Rabbil A'lamiin "Kuhimidiwa kote ni kwa
Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote."
***
11. Na lau kama Mwenyezi Mungu angeli wafanyia
watu haraka kuwaletea shari kama wanavyo jihimizia kuletewa kheri, bila
ya shaka wangelisha timiziwa ajali yao. Lakini tunawaacha wale wasio tumainia
kukutana nasi wakihangaika katika upotovu wao.
***
12. Na mtu akiguswa na shida hutuomba naye kaegesha
ubavu, au kakaa, au kasimama. Lakini tukimwondoshea shida yake huendelea
kama kwamba hakupata kutuomba tumwondoshee shida iliyo mpata. Ndio namna
hiyo wamepambiwa warukao mipaka yale waliyo kuwa wakiyatenda.
***
13. Na kwa yakini tumekwisha ziangamiza kaumu
za kabla yenu walipo dhulumu, na waliwajia Mitume wao kwa Ishara zilizo
wazi; lakini hawakuwa wenye kuamini. Ndio kama hivyo tunavyo walipa watu
wakosefu.
***
14. Kisha tukakufanyeni nyiye ndio wenye kushika
mahala pao baada yao katika ardhi ili tuone jinsi mtakavyo tenda.
***
15. Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi, wale
wasio taraji kukutana na Sisi husema: Lete Qur'ani isiyo kuwa hii, au ibadilishe.
Sema: Hainifalii mimi kuibadilisha kwa nitakavyo nafsi yangu. Mimi sifuati
ila ninayo funuliwa kwa Wahyi. Hakika mimi naogopa, nikimuasi Mola wangu
Mlezi, adhabu ya Siku iliyo kuu.
***
16. Sema: Mwenyezi Mungu angeli taka nisingeli
kusomeeni, wala nisingeli kujuvyeni. Kwani nalikwisha kaa nanyi umri mzima
kabla yake! Basi, je! Hamzingatii?
***
17. Basi ni nani aliye dhaalimu zaidi kuliko
yule anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu na akazikanusha Ishara zake? Hakika
hawafanikiwi wakosefu.
***
18. Nao, badala ya Mwenyezi Mungu, wanaabudu
wasio wadhuru wala kuwanufaisha, na wanasema: Hawa ndio waombezi wetu kwa
Mwenyezi Mungu! Sema: Je! Mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyo yajua ya katika
mbingu wala katika ardhi? Subhanahu wa Taa'la! Ametakasika na ametukuka
na hao wanao mshirikisha naye.
***
19. Wala watu hawakuwa ila Umma mmoja tu. Kisha
wakakhitalifiana. Na lau kuwa si neno lililo kwisha tangulia kutokana na
Mola wako Mlezi, hapana shaka hukumu ingeli kwisha katwa baina yao katika
hayo wanayo khitalifiana.
***
20. Na wanasema: Kwa nini hakuteremshiwa Ishara
kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Mambo ya ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu.
Basi nyinyi ngojeni, na mimi ni pamoja nanyi katika wanao ngojea.
***
21. Na tunapo waonjesha watu rehema baada ya
shida waliyo ipata, utawaona wana vitimbi kuzipangia Ishara zetu. Sema:
Mwenyezi Mungu ni Mwepesi zaidi wa kupanga. Hakika wajumbe wetu wanayaandika
mnayo yapanga.
***
22. Yeye ndiye anaye kuendesheni bara na baharini.
Hata mnapo kuwa majahazini na yakawa yanakwenda nao kwa upepo mzuri wakaufurahia,
upepo mkali ukawazukia, na yakawajia mawimbi kutoka kila upande, na wakaona
wamesha zongwa, basi hapo humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia niya:
Ukituokoa na haya bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa wanao shukuru.
***
23. Lakini akisha waokoa, mara wanafanya jeuri
tena katika nchi bila ya haki. Enyi watu! Jeuri zenu zitakudhuruni wenyewe.
Hii ni starehe ya maisha ya dunia tu. Kisha marejeo yenu ni kwetu, na hapo
tutakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
***
24. Hakika mfano wa maisha ya dunia ni kama maji
tuliyo yateremsha kutoka mbinguni, kisha yakachanganyika na mimea ya ardhi
wanayo ila watu na wanyama. Mpaka ardhi ilipo kamilika uzuri wake, na ikapambika,
na wenyewe wakadhani wamesha iweza, iliifikia amri yetu usiku au mchana,
tukaifanya kama iliyo fyekwa - kama kwamba haikuwapo jana. Namna hivi tunazipambanua
Ishara zetu kwa watu wanao fikiri.
***
25. Na Mwenyezi Mungu anaita kwendea Nyumba ya
Amani, na anamwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.
***
26. Kwa wafanyao wema ni wema na zaidi. Wala
vumbi halitawafunika nyuso zao, wala madhila. Hao ndio watu wa Peponi.
Humo watadumu.
***
27. Na wale walio chuma maovu, malipo ya uovu
ni mfano wake vile vile, na yatawafika madhila. Hawatakuwa na wa kuwalinda
na Mwenyezi Mungu. Nyuso zao kama kwamba zimefunikwa na vipande vya usiku
wa giza. Hao ndio watu wa Motoni, wao humo watadumu.
***
28. Na siku tutakapo wakusanya wote, kisha tutawaambia
walio shirikisha: Simameni mahali penu nyinyi na wale mlio wafanya washirika.
Kisha tutawatenga baina yao. Na hao walio washirikisha watasema: Nyinyi
hamkuwa mkituabudu sisi.
***
29. Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni shahidi baina
yetu na nyinyi. Hakika sisi tulikuwa hatuna khabari ya ibada yenu.
***
30. Huko kila mtu atayajua aliyo yatanguliza.
Na watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa Haki, na yote waliyo kuwa
wakiyazua yatawapotea.
***
31. Sema: Ni nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni
na kwenye ardhi? Au ni nani anaye miliki kusikia na kuona? Na nani amtoaye
hai kutoka maiti, na akamtoa maiti kutoka aliye hai? Na nani anaye yadabiri
mambo yote? Watasema: Allah, Mwenyezi Mungu. Basi sema: Je! Hamchi?
***
32. Basi huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi
wenu wa haki. Na kipo kitu gani baada ya haki, isipokuwa upotovu tu? Basi
huwaje mkageuzwa?
***
33. Ndio kama hivyo kauli ya Mola wako Mlezi
itakavyo wathibitikia wale walio potoka, ya kwamba hawatoamini.
***
34. Sema: Je! Yupo katika miungu yenu ya ushirikina
aliye anzisha kuumba viumbe, na kisha akavirejesha? Huwaje, basi, mkadanganywa?
***
35. Sema: Je! Yupo katika miungu yenu ya ushirikina
anaye ongoa kwendea Haki? Sema: Mwenyezi Mungu anaongoa kwendea Haki. Basi,
je, anaye stahiki kufuatwa ni yule Mwenye kuongoa kwendea Haki au asiye
ongoa ila aongozwe yeye? Basi nyinyi mna nini? Mnahukumu namna gani?
***
36. Na wengi wao hawafuati ila dhana tu. Na dhana
haifai kitu mbele ya haki. Hakika Mwenyezi Mungu anajua yote wanayo yatenda.
***
37. Na haiwezekani Qur'ani hii kuwa imetungwa
na haitoki kwa Mwenyezi Mungu. Lakini hii inasadikisha yaliyo tangulia,
na ni mfafanuo wa Kitabu kisicho na shaka ndani yake, kutokana na Mola
Mlezi wa viumbe vyote.
***
38. Je! Ndiyo wanasema ameizua? Sema: Hebu leteni
sura moja mfano wake na muwaite (kukusaidieni) muwawezao, isipo kuwa Mwenyezi
Mungu, ikiwa nyinyi mnasema kweli.
***
39.Bali wameyakanusha wasio yaelewa ilimu yake
kabla hayajawajia maelezo yake. Kadhaalika walio kabla yao walikanusha
vile vile. Basi angalia jinsi ulivyo kuwa mwisho wa madhaalimu hao.
***
40. Na miongoni mwao wapo wanao iamini, na miongoni
mwao wapo wasio iamini. Na Mola wako Mlezi anawajua vyema mafisadi.
***
41. Na wakikukanusha wewe, sema: Mimi nina a'mali
yangu, na nyinyi mna a'mali yenu. Nyinyi hamna jukumu kwa niyatendayo,
wala mimi sina jukumu kwa myatendayo.
***
42. Na wapo miongoni mwao wanao kusikiliza. Je,
wewe unaweza kuwafanya viziwi wasikie ijapo kuwa hawafahamu?
***
43. Na wapo miongoni mwao wanao kutazama. Je,
wewe utawaongoa vipofu ingawa hawaoni?
***
44. Hakika Mwenyezi Mungu hawadhulumu watu kitu
chochote; lakini watu wenyewe wanajidhulumu nafsi zao.
***
45. Na Siku atakapo wakusanya, itakuwa kama kwamba
hawakukaa ila saa moja tu ya mchana! Watatambuana. Hakika wamekhasirika
walio kanusha kukutana na Mwenyezi Mungu, wala hawakuwa wenye kuongoka.
***
46. Na vyovyote vile, tukikuonyesha baadhi ya
tunayo waahidi, au tukakufisha kabla yake, marejeo yao ni kwetu. Kisha
Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa wanayo yafanya.
***
47. Na kila umma una Mtume. Alipo wajia Mtume
wao walihukumiwa baina yao kwa uadilifu, wala hawakudhulumiwa.
***
48. Na wanasema: Lini ahadi hii, ikiwa mnasema
kweli?
***
49. Sema: Sijimilikii nafsi yangu shari wala
kheri ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Kila umma una muda wao walio wekewa.
Ukifika muda wao hawakawii hata saa moja wala hawatangulii.
***
50. Sema: Mwaonaje ikikufikieni hiyo adhabu yake
usiku au mchana, sehemu gani ya adhabu wanaihimiza wakosefu?
***
51. Tena je! Ikisha tokea mtaiamini? Je! Ndio
sasa tena? Na nyinyi mlikuwa mkiihimiza.
***
52. Kisha walio dhulumu wataambiwa: Onjeni adhabu
ya kudumu. Kwani mtalipwa isipo kuwa yale mliyo kuwa mkiyachuma?
***
53. Na wanakuuliza: Je! Ni kweli hayo? Sema:
Ehe! Naapa kwa Mola wangu Mlezi! Hakika hayo ni kweli, na wala nyinyi hamshindi!
***
54. Na lau kuwa kila nafsi iliyo dhulumu inamiliki
kila kiliomo duniani, bila ya shaka ingeli toa vyote kujikombolea. Na watakapo
iona adhabu wataficha majuto. Na patahukumiwa baina yao kwa uadilifu, nao
hawatadhulumiwa.
***
55. Jueni kuwa hakika vyote viliomo katika mbingu
na katika ardhi ni vya Mwenyezi Mungu. Jueni kuwa hakika ahadi ya Mwenyezi
Mungu ni ya haki. Lakini wengi wao hawajui.
***
56. Yeye ndiye anaye fufua na anaye fisha. Na
kwake mtarejeshwa.
***
57. Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa
Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema
kwa Waumini.
***
58. Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema
yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya.
***
59. Sema: Je! Mwaonaje zile riziki alizo kuteremshieni
Mwenyezi Mungu, nanyi mkafanya katika hizo nyengine haramu na nyengine
halali. Sema: Je! Mwenyezi Mungu amekuruhusuni, au mnamzulia Mwenyezi Mungu
tu?
***
60. Na nini dhana ya wanao mzulia Mwenyezi Mungu
kwa Siku ya Kiyama? Hakika Mwenyezi Mungu ana fadhila juu ya watu, lakini
wengi wao hawashukuru.
***
61. Na huwi katika jambo lolote, wala husomi
sehemu yoyote katika Qur'ani, wala hamtendi kitendo chochote ila Sisi huwa
ni mashahidi juu yenu mnapo shughulika nayo. Na hakifichikani kwa Mola
wako Mlezi chenye uzito hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu, wala
kidogo kuliko hicho wala kikubwa ila kimo katika Kitabu kilicho wazi.
***
62. Jueni kuwa vipenzi vya Mwenyezi Mungu hawatakuwa
na khofu wala hawatahuzunika.
***
63. Hao ni ambao wameamini na wakawa wanamcha
Mungu.
***
64. Wao wana bishara njema katika maisha ya dunia
na katika Akhera. Hapana mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu. Huko
ndiko kufuzu kukubwa.
***
65. Wala yasikuhuzunishe maneno yao. Hakika utukufu
wote ni wa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.
***
66. Jueni kuwa ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo
mbinguni na ardhinii. Na wala hawawafuati hao wanao waomba badala ya Mwenyezi
Mungu kuwa ni washirika wake. Wao hawafuati ila dhana tu, na hawasemi ila
uwongo.
***
67. Yeye ndiye aliye kujaalieni usiku mpate kutulia
humo, na mchana wa kuonea. Hakika katika haya zipo Ishara kwa watu wanao
sikia.
***
68. Wamesema: Mwenyezi Mungu ana mwana. Subhanahu,
Aliye takasika! Yeye ni Mkwasi, Mwenye Kujitosheleza. Vyote viliomo katika
mbingu na katika ardhi ni vyake peke yake. Nyinyi hamna uthibitisho wowote
wa haya! Mnamzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua?
***
69. Sema: Hao wanao mzulia uwongo Mwenyezi Mungu
hawatafanikiwa.
***
70. Hiyo ni starehe ya katika dunia tu, kisha
marejeo yao ni kwetu. Tena tutawaonjesha adhabu kali kwa sababu ya kukufuru
kwao.
***
71. Wasomee khabari za Nuhu alipo waambia watu
wake: Enyi watu wangu! Ikiwa kukaa kwangu nanyi na kukumbusha kwangu kwa
Ishara za Mwenyezi Mungu kunakutieni mashaka basi mimi namtegemea Mwenyezi
Mungu. Nanyi tengezeni mambo yenu pamoja na washirika wenu, na wala mambo
yenu yasifichikane kwenu. Kisha nihukumuni, wala msinipe muhula.
***
72. Lakini mkigeuka, basi mimi sikukuombeni ujira.
Ujira wangu hauko ila kwa Mwenyezi Mungu. Na nimeamrishwa niwe miongoni
mwa Waislamu.
***
73. Wakamkanusha. Basi tukamwokoa, pamoja na
walio kuwa naye, katika jahazi. Na tukawafanya wao ndio walio bakia, na
tukawazamisha walio zikanusha Ishara zetu. Basi angalia vipi ulikuwa mwisho
wa walio onywa.
***
74. Kisha baada yake tukawatuma Mitume kwa watu
wao. Nao wakawajia kwa Ishara zilizo wazi. Lakini hawakuwa wenye kuyaamini
waliyo yakanusha kabla yake. Ndio kama hivyo tunapiga muhuri juu ya nyoyo
za warukao mipaka.
***
75. Kisha baada yao tukamtuma Musa na Haruni
kwa Firauni na waheshimiwa wake, kwa Ishara zetu. Wakajivuna, na wakawa
watu wakosefu.
***
76. Basi ilipo wajia Haki kutoka kwetu walisema:
Hakika huu ni uchawi dhaahiri.
***
77. Akasema Musa: Mnasema hivi juu ya Haki ilipo
kujieni? Huu ni uchawi? Na wachawi hawafanikiwi!
***
78. Wakasema: Je! Umetujia ili utuachishe tuliyo
wakuta nayo baba zetu, na mpate nyinyi wawili ukubwa katika nchi? Wala
sisi hatukuaminini nyinyi.
***
79. Na Firauni akasema: Nileteeni kila mchawi
mjuzi!
***
80. Basi walipo kuja wachawi, Musa aliwaambia:
Tupeni mnavyo tupa!
***
81. Walipo tupa, Musa alisema: Mliyo leta ni
uchawi. Hakika Mwenyezi Mungu haitengenezi kazi ya waharibifu.
***
82. Na Mwenyezi Mungu huhakikisha Haki kwa maneno
yake, hata wanga chukia wakosefu
***
83. Basi hawakumuamini Musa isipo kuwa baadhi
ya vijana vya kaumu yake, kwa kumwogopa Firauni na wakuu wao wasiwatese.
Kwani hakika Firauni alikuwa jeuri katika nchi. Na kwa yakini alikuwa miongoni
mwa walio pita kiasi.
***
84. Na Musa alisema: Enyi watu wangu! Ikiwa nyinyi
mmemuamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni Yeye, ikiwa nyinyi ni Waislamu.
***
85. Wakasema: Tunamtegemea Mwenyezi Mungu. Ewe
Mola wetu Mlezi! Usitufanye wenye kutiwa misukosuko na hao watu madhaalimu.
***
86. Na utuokoe kwa rehema yako na watu makafiri.
***
87. Na tukampelekea Musa na ndugu yake wahyi
huu: Watengenezeeni majumba watu wenu katika Misri na zifanyeni nyumba
zenu ndio mwahali mwa ibada, na mshike Sala, na wabashirie Waumini.
***
88. Na Musa akasema: Mola wetu Mlezi! Hakika
wewe umempa Firauni na wakuu wake mapambo na mali katika maisha ya dunia.
Hivyo wanapoteza watu na Njia yako. Mola wetu Mlezi! Yafutilie mbali mali
yao na zifunge nyoyo zao, wasiamini mpaka waione adhabu chungu.
***
89. Mwenyezi Mungu akasema: Maombi yenu yamekubaliwa.
Basi simameni sawa sawa, wala msifuate njia za wale wasio jua.
***
90. Tukawavusha bahari Wana wa Israili, na Firauni
na askari wake wakawafuatia kwa dhulma na uadui. Hata Firauni alipo kuwa
anataka kuzama akasema: Naamini kuwa hapana mungu ila yule waliye muamini
Wana wa Israili, na mimi ni miongoni mwa walio nyenyekea!
***
91. Ala! Sasa? Na hali uliasi kabla yake na ukawa
miongoni mwa mafisadi!
***
92. Leo, basi, tutakuokoa kwa mwili wako, ili
uwe Ishara kwa ajili ya walio nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika
na Ishara zetu.
***
93. Na hakika tuliwaweka Wana wa Is raili kikao
chema, na tukawaruzuku vitu vizuri. Nao hawakukhitalifiana mpaka ilipo
wafikia ilimu. Hakika Mola wako Mlezi atahukumu baina yao Siku ya Kiyama
katika yale waliyo kuwa wakikhitalifiana.
***
94. Na ikiwa unayo shaka katika tuliyo kuteremshia,
basi waulize wasomao Kitabu kabla yako. Kwa yakini imekwisha kujia Haki
kutoka kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe miongoni mwa wenye shaka.
***
95. Na kabisa usiwe miongoni mwa wale wanao zikanusha
Ishara za Mwenyezi Mungu, usije kuwa katika walio khasiri.
***
96. Hakika wale ambao neno la Mola wako Mlezi
limekwisha thibitika juu yao, hawataamini,
***
97. Ijapo kuwa itawajia kila Ishara, mpaka waione
adhabu iliyo chungu.
***
98. Kwa nini usiwepo mji mmoja ukaamini na Imani
yake ikawafaa - isipo kuwa kaumu Yunus? Waliamini na Sisi tukawaondolea
adhabu ya hizaya katika maisha ya dunia, na tukawastarehesha kwa muda.
***
99. Angeli taka Mola wako Mlezi wangeli amini
wote waliomo katika ardhi. Je, wewe utawalazimisha watu kwa nguvu mpaka
wawe Waumini?
***
100. Na hawezi mtu kuamini ila kwa idhini ya
Mwenyezi Mungu. Naye hujaalia adhabu iwafike wasio tumia akili zao.
***
101. Sema: Angalieni yaliomo mbinguni na kwenye
ardhi! Na Ishara zote na maonyo hayawafai kitu watu wasio amini.
***
102. Basi, je! Wanangojea jingine ila kama yaliyo
tokea siku za watu walio pita kabla yao? Ngojeni! Nami ni pamoja nanyi
katika wanao ngoja.
***
103. Kisha Sisi huwaokoa Mitume wetu na walio
amini. Ndio kama hivyo, inatustahiki kuwaokoa Waumini.
***
104. Sema: Enyi watu! Ikiwa nyinyi mnayo shaka
katika Dini yangu, basi mimi siwaabudu mnao waabudu nyinyi badala ya Mwenyezi
Mungu. Lakini mimi namuabudu Mwenyezi Mungu anaye kufisheni. Na nimeamrishwa
niwe miongoni mwa Waumini.
***
105. Na uelekeze uso wako kwenye Dini ya Kweli,
wala usiwe katika washirikina.
***
106. Na wala usiwaombe wasio kuwa Mwenyezi Mungu
ambao hawakufai kitu wala hawakudhuru. Ukifanya hivyo basi utakuwa miongoni
mwa walio dhulumu.
***
107. Na Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara,
basi hapana wa kukuondolea ila Yeye. Na akikutakia kheri, basi hapana awezaye
kurudisha fadhila yake. Huifikisha kwa amtakaye katika waja wake, na Yeye
ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
***
108. Sema: Enyi watu! Haki imekwisha kukujieni
kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Basi anaye ongoka anaongoka kwa faida ya nafsi
yake, na anaye potea anapotea kwa khasara ya nafsi yake. Na mimi si mwakilishi
juu yenu.
***
109. Na wewe fuata yanayo funuliwa kwako kwa
wahyi. Na vumilia mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu, na Yeye ndiye mbora wa
mahakimu.
***
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com