Suratut Tawba iliteremka Madina katika mwaka wa tisa wa Hijra, yaani miaka
tisa baada ya Mtume s.a.w. kuhamia Madina. Akaichukua Sura hii Ali bin
Abi Talib r.a. kuwapelekea Waislamu katika Hija na akawasomea. Na amir,
yaani mwongozi, wa Hija hiyo alikuwa Abu Bakr Assidiq r.a. Na Aya zake
ni 129. Imeanzia kwa kujitenga Mwenyezi Mungu Mtukufu na washirikina. Na
kwa hivyo ikaitwa pia Sura ya Baraa-ah, yaani kujitenga, kutokuwa na dhima,
kutokuwa na jukumu. Na baada ya hayo ikataja utakatifu wa miezi mitakatifu,
na ahadi za washirikina, na ipasavyo kutimiza ahadi nao ikiwa wao hawajaivunja.
Na mwenye kuvunja ahadi yapasa kupigana naye. Na baada ya hayo ikabainisha
kuwa kiini cha kutaka kumkaribia Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kumuamini Yeye.
Na Imani haikamiliki ila akiwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapendwa
na Waumini kuliko kila kitu. Naye Subhanahu ametaja kuwa kujiona una nguvu
ndio kunapelekea kuwa mbali ushindi, na akaashiria mfano wa vita vya Hunayni.
Katika Sura hii wamepigiwa marfuku washirikina wasiingie katika Msikiti
Mtakatifu wa Makka, kwa kuwa wao ni najisi!
Na katika Sura hii imetajwa kupasa kuwapiga vita Mayahudi na Wakristo
mpaka watoe jizya, kodi ya kichwa, na imebainishwa idadi ya miezi mitakatifu.
Na humu imebainishwa dharura ya kutoka kwenda vitani kila vikinadiwa bila
ya kulegalega. Na humo imeashiriwa hukumu ya wanao bakia nyuma, na walemevu
wasio weza kwenda kupigana, na imebainishwa hali ya wanaafiki ambao wanatafuta
fitna kila wakati vinapo nadiwa vita. Na Mwenyezi Mungu akataja wanaafiki
wanavyo watendea Waumini wakati wa salama na vita.
Katika Sura hii iko amri ya kukata iliyo tangazwa kuwatia adabu wanaafiki.
Nayo ni kuwa Mtume s.a.w. asimsalie yeyote katika wanaafiki akifa.
Naye Subhanahu ametaja udhuru unao mstahikia mtu kubaki nyuma asende vitani.
Na pia Subhanahu ameeleza hali ya wale mabedui walio dhihirisha kuingia
katika Uislamu, au wakafuata hukumu zake, baada ya kuwa Uislamu umepata
nguvu. Na akaeleza kuwa hao mabedui wako kando kando ya Madina.
Na baada ya hayo ametaja hali za watu kwa mnasaba wa Imani. Na akataja
khabari ya Msikiti wa Madhara walio ujenga wanaafiki ili upuuzwe
Msikiti alio ujenga Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. Kisha Subhanahu akataja
sifa za Waumini walio wakweli katika Imani yao, na toba ya wale walio mkhalifu
Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w., na Mwenyezi Mungu akakubali toba hiyo,
kama alivyo taja Subhanahu wa Taa'la hali za watu katika kuzipokea Aya
za Qur'ani zinapo teremka. Na Subhanahu wa Taala akakhitimisha Sura hii
kwa kusema kuwa hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu amemteua Muhammad kwa kumpa
Utume, na kwamba yeye hawatakii shida hao alio tumwa kwao, na kwamba yeye
ni mpole na mwenye huruma kwao, na kwamba ikiwa wakigeuka basi Mwenyezi
Mungu anamtosheleza. (Angalia: Sura hii peke yake ndiyo haianzii kwa Bismillahi,
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu.)
1. Huku ni kujitoa Mwenyezi Mungu na Mtume wake
kwenye jukumu la maagano na mlio ahidiana nao katika washirikina.
***
2. Basi tembeeni katika nchi miezi mine, na jueni
kwamba nyinyi hamwezi kumshinda Mwenyezi Mung, na kwamba Mwenyezi Mungu
ndiye anaye wahizi makafiri.
***
3. Na ni tangazo kutokana na Mwenyezi Mungu na
Mtume wake kwa wote siku ya Hija Kubwa kwamba Mwenyezi Mungu na Mtume wake
hawana jukumu lolote kwa washirikina. Basi mkitubu itakuwa kheri kwenu,
na mkigeuka basi jueni kuwa nyinyi hamumshindi Mwenyezi Mungu. Na wabashirie
makafiri kuwa watapata adhabu chungu.
***
4. Isipo kuwa washirikina ambao mliahidiana nao
kisha wasikupunguzieni chochote, wala hawakumsaidia yeyote dhidi yenu,
basi hao watimizieni ahadi yao mpaka muda wao. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda
wacha-Mungu.
***
5. Na ikisha miezi mitukufu basi wauweni washirikina
popote mwakutapo, na washikeni na wazungukeni, na wavizieni katika kila
njia. Lakini wakitubu, wakashika Sala, na wakatoa Zaka, basi waachilieni.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
***
6. Na ikiwa mmoja wapo katika washirikina akikuomba
ulinzi, basi mpe ulinzi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu. Kisha mfikishe
pahala pake pa amani. Haya ni kwa kuwa hao ni watu wasiojua kitu.
***
7. Itakuwaje iwepo ahadi na washirikina mbele ya
Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume wake, ila wale mlio ahidiana nao kwenye
Msikiti Mtakatifu? Basi maadamu wanakwenda nanyi sawa, nanyi pia nendeni
sawa nao. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wachamngu
***
8. Itakuwaje! Nao wakikushindeni hawatazami kwenu
udugu wala ahadi. Wanakufurahisheni kwa midomo yao tu, na nyoyo zao zinakataa
hayo. Na wengi wao ni wapotovu.
***
9. Wamenunua thamani ndogo kwa Ishara za Mwenyezi
Mungu, na wakazuilia watu na Njia yake. Hakika hao ni maovu waliyo kuwa
wakiyatenda.
***
10. Hawatazami kwa Muumini udugu wala ahadi; basi
hao ndio warukao mipaka.
***
11. Basi wakitubu na wakashika Sala na wakatoa
Zaka, basi ni ndugu zenu katika Dini. Na tunazichambua Aya kwa watu wajuao.
***
12. Na wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao,
na wakatukana Dini yenu, basi piganeni na waongozi wa ukafiri. Hakika hao
hawana viapo vya kweli. Huenda (kwa hayo) wakaacha.
***
13. Je, hamtapigana na watu walio vunja viapo
vyao na wakawa na hamu ya kumfukuza Mtume, nao ndio walio kuanzeni mara
ya kwanza? Je, mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumwogope,
ikiwa nyinyi ni Waumini.
***
14. Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa
mikono yenu, na awahizi na akunusuruni muwashinde, na avipoze vifua vya
kaumu ya Waumini,
***
15. Na aondoe hasira ya nyoyo zao. Na Mwenyezi
Mungu humkubalia toba ya amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye
hikima.
***
16. Je, mlidhani kuwa mtaachwa tu, bila ya Mwenyezi
Mungu kuwajuulisha wale walio pigana Jihadi kati yenu, na wala hawakumfanya
mwendani wao isipo kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Waumini wenziwe?
Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda.
***
17. Haiwi kuwa makafiri ndio waamirishe misikiti
ya Mwenyezi Mungu, hali wanajishuhudishia wenyewe ukafiri. Hao ndio ambao
vitendo vyao vimeharibika, na katika Moto watadumu.
***
18. Hakika wanao amirisha misikiti ya Mwenyezi
Mungu ni wale wanao muamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na wakashika
Sala, na wakatoa Zaka, na wala hawamchi ila Mwenyezi Mungu. Basi huenda
hao wakawa katika waongofu.
***
19. Je, mnafanya kuwanywesha maji Mahujaji na
kuamirisha Msikiti Mtakatifu ni sawa na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu,
na Siku ya Mwisho, na akapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Hawawi
sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
***
20. Wale walio amini, na wakahama, na wakapigana
Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao, hao wana
cheo kikubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufuzu.
***
21. Mola wao Mlezi anawabashiria rehema zitokazo
kwake, na radhi, na Bustani ambazo humo watapata neema za kudumu.
***
22. Watadumu humo milele. Hakika kwa Mwenyezi
Mungu yapo malipo makubwa.
***
23. Enyi mlio amini! Msiwafanye baba zenu na ndugu
zenu kuwa vipenzi vyenu ikiwa wanastahabu ukafiri kuliko Imani. Na katika
nyinyi atakaye wafanya hao ndio vipenzi vyake, basi hao ndio madhaalimu.
***
24. Sema: Ikiwa baba zenu, na wenenu, na ndugu
zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na mali mliyo yachuma, na biashara mnazo
ogopa kuharibika, na majumba mnayo yapenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko
Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Jihadi katika Njia yake, basi ngojeni mpaka
Mwenyezi Mungu alete amri yake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.
***
25. Hakika Mwenyezi Mungu amekunusuruni katika
mapigano mengi, na siku ya Hunayni ambapo wingi wenu ulikupandisheni kichwa,
lakini haukukufaeni kitu. Na ardhi ikawa dhiki kwenu juu ya upana wake.
Kisha mkageuka mkarudi nyuma.
***
26. Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha utulivu wake
juu ya Mtume wake na juu ya Waumini. Na akateremsha majeshi ambayo hamkuyaona,
na akawaadhibu wale walio kufuru. Na hayo ndiyo malipo ya makafiri.
***
27. Kisha baada ya hayo Mwenyezi Mungu atawasamehe
awatakao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
***
28. Enyi mlio amini! Hakika washirikina ni najsi,
kwa hivyo wasiukaribie Msikiti Mtakatifu baada ya mwaka wao huu. Na ikiwa
mnakhofia umasikini, basi Mwenyezi Mungu atakutajirisheni kwa fadhila yake
akipenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
***
29. Piganeni na wasio muamini Mwenyezi Mungu wala
Siku ya Mwisho, wala hawaharimishi alivyo harimisha Mwenyezi Mungu na Mtume,
wala hawashiki Dini ya Haki, miongoni mwa walio pewa Kitabu, mpaka watoe
kodi kwa khiari yao, hali wamet'ii.
***
30. Na Mayahudi wanasema: Uzeir ni mwana wa Mungu.
Na Wakristo wanasema: Masihi ni mwana wa Mungu. Hiyo ndiyo kauli yao kwa
vinywa vyao. Wanayaiga maneno ya walio kufuru kabla yao. Mwenyezi Mungu
awaangamize! Wanageuzwa namna gani hawa!
***
31. Wamewafanya makuhani wao na wamonaki wao kuwa
ni marabi badala ya Mwenyezi Mungu, na pia Masihi bin Maryamu. Na wala
hawakuamrishwa isipo kuwa wamuabudu Mungu Mmoja, hapana mungu ila Yeye.
Subhanahu, Ametakasika na hayo wanayo mshirikisha nayo.
***
32. Wanataka kuizima Nuru ya Mwenyezi Mungu kwa
vinywa vyao, na Mwenyezi Mungu anakataa ila aitimize Nuru yake ijapo kuwa
makafiri watachukia.
***
33. Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu
na Dini ya Haki ipate kushinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia.
***
34. Enyi mlio amini! Hakika wengi katika makuhani
na wamonaki wanakula mali za watu kwa baat'ili na wanazuilia Njia ya Mwenyezi
Mungu. Na wanao kusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia
ya Mwenyezi Mungu, wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu.
***
35. Siku zitapo tiwa moto katika Moto wa Jahannamu,
na kwazo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, wakaambiwa:
Haya ndiyo mlio jilimbikia nafsi zenu, basi onjeni mliyo kuwa mkilimbika.
***
36. Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni
miezi kumi na mbili katika hukumu ya Mwenyezi Mungu tangu alipo umba mbingu
na ardhi. Katika hiyo iko mine mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa.
Basi msidhulumu nafsi zenu humo. Na piganeni na washirikina wote kama wao
wnavyo pigana nanyi nyote. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamngu.
***
37. Bila ya shaka kuakhirisha (miezi) ni kuzidi
katika kukufuru; kwa hayo hupotezwa walio kufuru. Wanauhalalisha mwaka
mmoja na kuharimisha mwaka mwingine, ili wafanye kuwa sawa idadi ya ile
(miezi) aliyo itukuza Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo huhalalisha alivyo viharimisha
Mwenyezi Mungu. Wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao hivi. Na Mwenyezi Mungu
hawaongoi watu makafiri.
***
38. Enyi mlio amini! Mna nini mnapo ambiwa: Nendeni
katika Njia ya Mwenyezi Mungu, mnajitia uzito katika ardhi? Je, mmeridhia
maisha ya dunia kuliko ya Akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia kulinganisha
na ya Akhera ni chache.
***
39. Kama hamwendi atakuadhibuni adhabu chungu,
na atawaleta watu wengine, wala nyinyi hamtamdhuru chochote. Na Mwenyezi
Mungu ni Muweza wa kila kitu.
***
40. Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Mwenyezi
Mungu alikwisha mnusuru walipo mtoa walio kufuru, naye ni wa pili katika
wawili walipo kuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike.
Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu
wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyo yaona, na akalifanya neno la
walio kufuru kuwa chini, na Neno la Mwenyezi Mungu kuwa ndilo juu. Na Mwenyezi
Mungu ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima.
***
41. Nendeni mtoke, mkiwa wepesi na wazito, na
piganeni Jihadi kwa mali yenu na nafsi zenu katika Njia ya Mwenyezi Mungu.
Haya ni kheri kwenu mkiwa mnajua.
***
42. Na lau ingeli kuwa ipo faida ya papo kwa papo,
na safari yenyewe ni fupi, wangeli kufuata. Lakini wameona ni mbali na
kuna mashaka. Nao wataapa kwa Mwenyezi Mungu: Tungeli weza bila ya shaka
tungeli toka pamoja nanyi. Wanaziangamiza nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu
anajua kuwa hakika hao ni waongo.
***
43. Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini ukawapa
ruhusa kabla ya kubainikia kwako wanao sema kweli, na ukawajua waongo?
***
44. Hawatakuomba ruhusa wale wanao muamini Mwenyezi
Mungu na Siku ya Mwisho, wasende kupigana Jihadi kwa mali yao na nafsi
zao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwajua wachamngu.
***
45. Wasio muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho
na nyoyo zao zikatia shaka, hao tu ndio wanao kutaka ruhusa. Basi hao wanataradadi
katika shaka zao.
***
46. Na ingeli kuwa kweli walitaka kutoka bila
ya shaka wangeli jiandalia maandalio, lakini Mwenyezi Mungu kachukia kutoka
kwao, na kwa hivyo akawazuia na ikasemwa: Kaeni pamoja na wanao kaa!
***
47. Lau wangeli toka nanyi wasingeli kuzidishieni
ila mchafuko, na wange tanga tanga kati yenu kukutilieni fitna. Na miongoni
mwenu wapo wanao wasikiliza. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu.
***
48. Tangu zamani walitaka kukutilieni fitna, na
wakakupindulia mambo juu chini, mpaka ikaja Haki na ikadhihirika amri ya
Mwenyezi Mungu, na wao wamechukia.
***
49. Na miongoni mwao wapo wanao sema: Niruhusu
wala usinitie katika fitina. Kwa yakini wao hivyo wamekwisha tumbukia katika
fitina. Na hakika Jahannamu imewazunguka.
***
50. Ukikupata wema unawachukiza, na ukikusibu
msiba, wao husema: Sisi tuliangalia mambo yetu vizuri tangu kwanza. Na
hugeuka kwenda zao nao wamefurahi.
***
51. Sema: Halitusibu ila alilo tuandikia Mwenyezi
Mungu. Yeye ndiye Mola wetu Mlinzi. Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu
tu!
***
52. Sema: Hivyo mnatutazamia litupate lolote isipo
kuwa moja katika mema mawili? Na sisi tunakutazamieni kuwa Mwenyezi Mungu
akufikishieni adhabu itokayo kwake, au kutokana na mikono yetu. Basi ngojeni,
nasi tunangoja pamoja nanyi.
***
53. Sema: Toeni mkipenda msipende. Hakitopokelewa
kitu kwenu, kwani nyinyi ni watu wapotovu.
***
54. Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao ila
kwa kuwa walimkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawaji kwenye Sala
ila kwa uvivu, wala hawatoi michango ila nao wamechukia.
***
55. Yasikufurahishe mali yao wala wana wao. Hakika
Mwenyezi Mungu anataka kuwaadhibu kwayo hapa duniani, na zitoke roho zao
na hali wao ni makafiri.
***
56. Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao ni
katika nyinyi, wala wao si katika nyinyi. Lakini ni watu wanao ogopa.
***
57. Lau kama wangeli pata pa kukimbilia au mapango
au pahala pa kuingia basi wangeli fyatuka mbio kuelekea huko.
***
58. Na miongoni mwao wapo wanao kusengenya katika
kugawa sadaka. Wanapo pewa wao huridhika. Na wakito pewa hukasirika.
***
59. Na laiti wao wangeli ridhia kile alicho wapa
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosheleza,
Mwenyezi Mungu atatupa katika fadhila yake - na pia Mtume wake; hakika
sisi ni wenye kumtaka Mwenyezi Mungu!
***
60. Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini,
na wanao zitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa,
na wenye madeni, na katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni
waajibu ulio faridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua
Mwenye hikima.
***
61. Na miongoni mwao wapo wanao muudhi Nabii na
kusema: Yeye huyu ni sikio tu. Sema: Basi ni sikio la kheri kwenu. Anamuamini
Mwenyezi Mungu, na ana imani na Waumini, naye ni rehema kwa wanao amini
miongoni mwenu. Na wanao muudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu watapata adhabu
chungu.
***
62. Wanakuapieni Mwenyezi Mungu ili kukuridhisheni
nyinyi, hali ya kuwa wanao stahiki zaidi kuridhishwa ni Mwenyezi Mungu
na Mtume wake, lau kama wao ni Waumini.
***
63. Je, hawajui ya kwamba anaye shindana na Mwenyezi
Mungu na Mtume wake, basi huyo atapata Moto wa Jahannamu adumu humo? Hiyo
ndiyo hizaya kubwa.
***
64. Wanaafiki wanaogopa isije teremshwa Sura itakayo
watajia yaliyomo katika nyoyo zao. Sema: Fanyeni mzaha! Hakika Mwenyezi
Mungu atayatoa nje hayo mnayo yaogopa.
***
65. Na ukiwauliza, wanasema: Sisi tulikuwa tukipiga
porojo na kucheza tu. Sema: Mlikuwa mkimfanyia maskhara Mwenyezi Mungu
na Ishara zake na Mtume wake?
***
66. Msitoe udhuru; mmekwisha kufuru baada ya kuamini
kwenu! Tukilisamehe kundi moja kati yenu, tutaliadhibu kundi jingine kwa
kuwa wao ni wakosefu.
***
67. Wanaume wanaafiki na wanawake wanaafiki, wote
ni hali moja. Huamrisha maovu na huyakataza mema, na huifumba mikono yao.
Wamemsahau Mwenyezi Mungu, basi na Yeye pia amewasahau. Hakika wanaafiki
ndio wapotofu.
***
68. Mwenyezi Mungu amewaahidi wanaafiki wanaume
na wanaafiki wanawake na makafiri Moto wa Jahannamu kudumu humo. Hayo yanawatosha,
na Mwenyezi Mungu amewalaani; nao wana adhabu milele.
***
69. Ni kama wale walio kuwa kabla yenu. Walikuwa
wana nguvu na mali na watoto zaidi kuliko nyinyi. Basi walistarehea fungu
lao, na nyinyi mnastarehea fungu lenu, kama walivyo starehe kwa fungu lao
wale walio kuwa kabla yenu. Na nyinyi mkazama katika maovu kama wao walivyo
zama. Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika katika dunia na Akhera;
na hao ndio walio khasiri.
***
70. Je, hazikuwafikia khabari za walio kuwa kabla
yao - kaumu ya Nuhu, na A'ad, na Thamud, na kaumu ya Ibrahim, na watu wa
Madyana, na miji iliyo pinduliwa chini juu? Mitume wao waliwafikia kwa
hoja zilizo wazi. Basi Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, walakini
wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe.
***
71. Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao
kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika
Sala, na hutoa Zaka, na humt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi
Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye
hikima.
***
72. Mwenyezi Mungu amewaahidi Waumini wanaume
na Waumini wanawake Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na makaazi
mema katika Bustani za kudumu, na Radhi za Mwenyezi Mungu ndio kubwa kuliko
yote. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
***
73. Ewe Nabii! Pambana na makafiri na wanaafiki,
na wakazanie. Na makaazi yao ni Jahannamu, na huo ndio mwisho mbaya.
***
74. Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hawakusema;
nao wamekwisha sema neno la ukafiri, na wakakufuru baada ya kusilimu kwao.
Na wakajihimu kufanya ambayo hawakuweza kuyafikia. Na hawakuchukia ila
kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake amewatajirisha kutokana na fadhila zake.
Wakitubu itakuwa kheri kwao, na wakigeuka Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu
chungu duniani na Akhera. Na wala hawana katika ardhi mlinzi wala wa kuwanusuru.
***
75. Na miongoni mwao wapo walio muahidi Mwenyezi
Mungu kwa kusema: Akitupa katika fadhila yake hapana shaka tutatoa sadaka,
na tutakuwa katika watendao mema.
***
76. Alipo wapa katika fadhila yake wakaifanyia
ubakhili na wakageuka, na huku wakipuuza.
***
77. Basi akawalipa unaafiki kuutia nyoyoni mwao
mpaka Siku watapo kutana naye, kwa sababu ya kuwa walimkhalifu Mwenyezi
Mungu katika yale waliyo muahidi, na kwa sababu ya kusema kwao uwongo.
***
78. Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anajua siri
zao na minong'ono yao, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua sana
ya ghaibu?
***
79. Wale wanao wabeuwa Waumini wanao toa sadaka
nyingi na wasio nacho cha kutoa ila kadri ya juhudi yao, basi huwakejeli.
Mwenyezi Mungu atawakejeli wao! Nao watapata adhabu chungu!
***
80. Waombee msamaha au usiwaombee. Hata ukiwaombea
msamaha mara sabiini, Mwenyezi Mungu hatawasamehe. Hayo ni kwa sababu ya
kuwa wao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi
watu wapotofu.
***
81. Walifurahi walio achwa nyuma kwa kule kubakia
kwao nyuma na kumuacha Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walichukia kupigana
Jihadi kwa mali zao na nafsi zao, na wakasema: Msitoke nje katika joto!
Sema: Moto wa Jahannamu una joto zaidi, laiti wangeli fahamu!
***
82. Basi nawacheke kidogo; watalia sana. Hayo
ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyachuma.
***
83. Basi Mwenyezi Mungu akikurudisha kwenye kikundi
kimoja miongoni mwao - na wakakutaka idhini ya kutoka - sema: Nyinyi hamtatoka
pamoja nami kabisa, wala hamtapigana na adui pamoja nami. Nyinyi mliridhia
kukaa nyuma mara ya kwanza, basi kaeni pamoja na hao watakao bakia nyuma.
***
84. Wala usimsalie kabisa yeyote katika wao akifa,
wala usisimame kaburini kwake. Hakika hao wamemkataa Mwenyezi Mungu na
Mtume wake, na wakafa na hali ni wapotofu.
***
85. Wala zisikushitue mali zao na watoto wao.
Mwenyezi Mungu anataka kuwaadhibu kwa hayo katika dunia; na zitoke roho
zao na hali wao ni makafiri.
***
86. Na inapo teremshwa Sura isemayo: Muaminini
Mwenyezi Mungu na piganeni Jihadi pamoja na Mtume wake, wale wenye nguvu
miongoni mwao hukutaka ruhusa na husema: Tuache tuwe pamoja na wanao kaa
nyuma!
***
87. Wameridhia kuwa pamoja na wabakiao nyuma,
na nyoyo zao zikapigwa muhuri; kwa hivyo hawafahamu.
***
88. Lakini Mtume na wale walio amini pamoja naye
waliwania Jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio watakao pata kheri
nyingi, na hao ndio wenye kufanikiwa.
***
89. Mwenyezi Mungu amewatengenezea Bustani zipitazo
mito kati yake, wadumu humo. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
***
90. Na walikuja wenye kutoa udhuru katika Mabedui
ili wapewe ruhusa, na wakakaa wale walio mwambia Mwenyezi Mungu na Mtume
wake uwongo. Itawafika walio kufuru katika wao adhabu chungu.
***
91. Hapana lawama kwa wanyonge, wagonjwa, na wasio
pata cha kutumia, maadamu wanamsafia niya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Hapana njia ya kuwalaumu wanao fanya wema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe Mwenye kurehemu.
***
92. Wala wale walio kujia ili uwachukue ukasema:
Sina kipando cha kukuchukueni. Tena wakarudi na macho yao yanamiminika
machozi kwa huzuni ya kukosa cha kutoa.
***
93. Ipo njia ya kuwalaumu wale wanao kuomba ruhusa
wasende vitani na hali wao ni matajiri. Wameridhia kuwa pamoja na wanao
bakia nyuma. Na Mwenyezi Mungu amewapiga muhuri juu ya nyoyo zao. Kwa hivyo
hawajui.
***
94. WATAKUTOLEENI UDHURU mtapo warudia. Sema:
Msitoe udhuru; hatukuaminini. Mwenyezi Mungu amekwisha tueleza khabari
zenu. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wataviona vitendo vyenu. Kisha mtarudishwa
kwa Mjuzi wa ya siri na ya dhaahiri; naye atakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
***
95. Watakuapieni kwa Mwenyezi Mungu mtakapo rudi
kwao ili muwaachilie mbali. Basi waachilieni mbali. Hakika hao ni najsi,
na makaazi yao ni Jahannamu, kuwa ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
***
96. Wanakuapieni ili muwe radhi nao. Basi hata
mkiwa radhi nao nyiye, Mwenyezi Mungu hawi radhi na watu wapotofu.
***
97. Mabedui wamezidi sana katika ukafiri na unaafiki,
na wameelekea zaidi kutojua mipaka ya aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu juu
ya Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.
***
98. Na katika Mabedui hao wapo wanao fikiri kuwa
wanayo yatoa ni gharama ya bure, na wanakungojeleeni mambo yakugeukieni.
Mageuko maovu yatakuwa juu yao! Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye
kujua.
***
99. Na katika Mabedui wapo wanao muamini Mwenyezi
Mungu na Siku ya Mwisho, na wanaitakidi kuwa wanayo yatoa ndiyo ya kuwasogeza
kwa Mwenyezi Mungu na ya kuwapatia dua za Mtume. Naam! Hayo ni kweli mambo
ya kuwasogeza. Mwenyezi Mungu atawaingiza katika rehema yake. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye maghfira Mwenye kurehemu.
***
100. Na wale walio tangulia, wa kwanza, katika
Wahajiri na Ansari, na walio wafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika
nao, na wao wameridhika naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati
yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
***
101. Na katika mabedui walio jirani zenu wamo
wanaafiki; na katika wenyeji wa Madina pia wapo walio bobea katika unaafiki.
Wewe huwajui. Sisi tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa
kwenye adhabu kubwa.
***
102. Na wengine walikiri dhambi zao, wakachanganya
vitendo vyema na vingine viovu. Asaa Mwenyezi Mungu akapokea toba zao.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
***
103. Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe
na uwatakase kwazo, na uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
***
104. Je! Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anapokea
toba ya waja wake, na anazikubali sadaka, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi
wa kupokea toba na Mwenye kurehemu?
***
105. Na sema: Tendeni vitendo. Na Mwenyezi Mungu,
na Mtume wake, na Waumini wataviona vitendo vyenu. Na mtarudishwa kwa Mwenye
kujua siri na dhaahiri; naye atakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
***
106. Na wapo wengine wanangojea amri ya Mwenyezi
Mungu - ama atawaadhibu au atawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua
Mwenye hikima.
***
107. Na wapo walio jenga msikiti kwa ajili ya
madhara na ukafiri na kuwafarikisha Waumini, na pa kuvizia kwa walio mpiga
vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake hapo kabla. Na bila ya shaka wataapa
kwamba: Hatukukusudia ila wema tu. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa wao
ni waongo.
***
108. Usisimame kwenye msikiti huo kabisa. Msikiti
ulio jengwa juu ya msingi wa uchamngu tangu siku ya mwanzo unastahiki zaidi
wewe usimame ndani yake. Humo wamo watu wanao penda kujitakasa. Na Mwenyezi
Mungu anawapenda wanao jitakasa.
***
109. Je! Mwenye kuweka msingi wa jengo lake juu
ya kumcha Mwenyezi Mungu na radhi zake ni bora au mwenye kuweka msingi
wa jengo lake juu ya ukingo wa shimo linalo burugunyika, na likaburugunyika
naye katika Moto wa Jahannamu? Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
***
110. Na jengo lao hilo walilo lijenga litakuwa
sababu ya kutia wasiwasi nyoyoni mwao mpaka nyoyo zao hizo zikatike vipande
vipande. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
***
111. Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini
nafsi zao na mali zao kwa kuwa wao watapata Pepo. Wanapigana katika Njia
ya Mwenyezi Mungu - wanauwa na wanauwawa. Hii ni ahadi aliyo jilazimisha
kwa Haki katika Taurati na Injili na Qur'ani. Na nani atimizae ahadi kuliko
Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliyo fanya naye. Na huko
ndiko kufuzu kukubwa,
***
112. (Kwa) wanao tubia, wanao abudu, wanao himidi,
wanao kimbilia kheri, wanao rukuu, wanao sujudu, wanao amrisha mema na
wanao kataza maovu, na wanao linda mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na wabashirie
Waumini.
***
113. Haimpasii Nabii na wale walio amini kuwatakia
msamaha washirikina, ijapo kuwa ni jamaa zao, baada ya kwisha bainika kuwa
hao ni watu wa Motoni.
***
114. Wala haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba
yake ila kwa sababu wa ahadi aliyo fanya naye. Lakini ilipo mbainikia kwamba
yeye ni adui ya Mwenyezi Mungu, alijiepusha naye. Hakika Ibrahim alikuwa
mwingi wa kuomba, mnyenyekevu, mvumilivu.
***
115. Na haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwahisabu watu
kuwa wamepotea baada ya kwisha waongoza mpaka awabainishie ya kujiepusha
nayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
***
116. Hakika Mwenyezi Mungu anao ufalme wa mbingu
na ardhi; huhuisha na hufisha. Nanyi hamna Mlinzi wala Msaidizi isipo kuwa
Mwenyezi Mungu.
***
117. Mwenyezi Mungu amekwisha pokea toba ya Nabii
na Wahajiri na Ansari walio mfuata katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia
nyoyo za baadhi yao kugeuka. Basi akapokea toba yao, kwani hakika Yeye
kwao wao ni Mpole na ni Mwenye kuwarehemu.
***
118. Na pia wale watatu walio achwa nyuma hata
dunia wakaiona dhiki juu ya ukunjufu wake, na nafsi zao zikabanika, na
wakayakinika kuwa hapana pa kumkimbia Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwake Yeye.
Kisha akawaelekea kwa rehema yake ili nao waendelee kutubu. Hakika Mwenyezi
Mungu ndiye Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.
***
119. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu,
na kuweni pamoja na wakweli.
***
120. Haiwafalii watu wa Madina na Mabedui walio
jirani zao kubakia nyuma wasitoke na Mtume, wala kujipendelea nafsi zao
kuliko yeye. Hayo ni kwa kuwa hakiwapati kiu, wala machofu, wala njaa,
kwa ajili ya Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawendi mahali panapo waghadhibisha
makafiri, wala hakiwapati chochote kutokana na maadui, ila huandikiwa kuwa
ni kitendo chema. Hakika Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa wanao fanya
mema.
***
121. Wala hawatoi cha kutoa kidogo wala kikubwa,
wala hawalivuki bonde, ila huandikiwa, ili Mwenyezi Mungu awalipe bora
ya waliyo kuwa wakiya- tenda.
***
122. Wala haiwafalii Waumini kutoka wote. Lakini
kwa nini hawatoki baadhi katika kila kundi miongoni mwao, wakajifunze vyema
Dini, na kisha waje kuwaonya wenzao watakapo warejea, ili wapate kujihadharisha?
***
123. Enyi mlio amini! Piganeni na wale makafiri
walio karibu yenu, na wakute ugumu kwenu. Na jueni ya kwamba Mwenyezi Mungu
yu pamoja na wacha- Mngu.
***
124. Na inapo teremshwa Sura wapo miongoni mwao
wasemao: Ni nani miongoni mwenu Sura hii imemzidishia Imani? Ama wale walio
amini inawazidishia Imani, nao wanafurahi.
***
125. Ama wale wenye maradhi katika nyoyo zao,
basi inawazidishia uovu juu ya uovu wao; na wanakufa hali ni makafiri.
***
126. Je! Hawaoni ya kwamba wanatiwa mtihanini
kila mwaka mara moja au mara mbili? Kisha hawatubu, wala hawakumbuki.
***
127. Na ikiteremka Sura hutazamana wao kwa wao,
(kama kwamba wanasema:) Je! Yuko mtu anakuoneni? Kisha hugeukilia mbali.
Mwenyezi amezigeuza nyoyo zao kwa kuwa hao ni watu wasio fahamu.
***
128. Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana
na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni
sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.
***
129. Basi wakigeuka, wewe sema: Mwenyezi Mungu
ananitosheleza. Hapana mungu isipokuwa Yeye tu. Mimi namtegemea Yeye, na
Yeye ndiye Mola Mlezi wa Kiti Kikuu cha Enzi.
***
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com