Surat Al Anfaal hii imeteremka Madina. Aya zake ni 75. Mwenyezi Mungu aliye
takasika na kutukuka, amebainisha katika Sura hii baadhi ya hukumu za vita,
na mambo yanayo pelekea vita, na sababu za ushindi, na makamo ya nguvu
za moyo zinazo pelekea kushinda, na hukumu za ngawira za vita, na wakati
gani kuchukua mateka. Na Mwenyezi Mungu kwa hikima yake amekusanya humu
hukumu za kisharia. Sura hii inaeleza kisa cha Vita vya Badri, na baadhi
ya yaliyo kuwa kabla yake, na kuashiria sababu zilizo sabibisha hivyo vita,
nazo ni kutoka makafiri washirikina Makka kumwendea Nabii s.a.w.. Na humu
Mwenyezi Mungu anataja kujitayarisha kwa vita, na kupasa kuelekea salama
na amani ikiwa maadui wanaelekea kutaka salama. Na Sura hii tukufu inamalizikia
kubainisha urafiki wa Waumini, wao kwa wao; na kuwawajibikia Waumini kuihama
nchi inayo waonea na kuwafanya wanyonge, ili wende kuwaunga mkono Waumini
wenzao katika juhudi ya kutukuza Uislamu na Waislamu.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA, MWENYE KUREHEMU
1. Wanakuuliza juu ya Ngawira. Sema: Ngawira ni
ya Mwenyezi Mungu na Mtume. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na suluhisheni mambo
baina yenu, na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni Waumini.
***
2. Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi
Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanapo somewa Aya zake huwazidisha Imani,
na wakamtegemea Mola wao Mlezi.
***
3. Hao ambao wanashika Sala na wanatoa katika yale
tunayo waruzuku.
***
4. Hao kweli ndio Waumini. Wao wana vyeo, na maghfira,
na riziki bora, kwa Mola wao Mlezi. ***
5. Kama Mola wako Mlezi alivyo kutoa nyumbani kwako
kwa Haki, na hakika kundi moja la Waumini linachukia.
***
6. Wanajadiliana nawe kwa jambo la Haki baada ya
kwisha bainika, kama kwamba wanasukumwa kwenye mauti nao wanaona.
***
7. Na Mwenyezi Mungu alipo kuahidini kuwa moja
katika makundi mawili ni lenu. Nanyi mkapenda lisilo na nguvu ndio liwe
lenu; na Mwenyezi Mungu anapenda ahakikishe Haki kwa maneno yake, na aikate
mizizi ya makafiri.
***
8. Ili ahakikishe Haki na auvunje upotovu na wangachukia
wakosefu.
***
9. Mlipo kuwa mkimuomba msaada Mola wenu Mlezi,
naye akakujibuni kuwa: Kwa yakini Mimi nitakusaidieni kwa Malaika elfu
wanao fuatana mfululizo.
***
10. Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa
ni bishara na ili nyoyo zenu zituwe. Na haupatikani ushindi ila kutoka
kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.
***
11. Alipo kufunikeni kwa usingizi uwe ni uaminisho
kutoka kwake, na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni
kwayo na kukuondoleeni uchafu wa Shet'ani, na kuzipa nguvu nyoyo zenu,
na kuitia imara miguu yenu.
***
12. Mola wako Mlezi alipo wafunulia Malaika: Hakika
Mimi ni pamoja nanyi, basi watieni nguvu walio amini. Nitatia woga katika
nyoyo za walio kufuru. Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila
ncha za vidole.
***
13. Hayo ni kwa sababu wamemuasi Mwenyezi Mungu
na Mtume wake. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi Mwenyezi
Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
***
14. Ndio hivyo! Basi ionjeni! Na bila ya shaka
makafiri wana adhabu ya Moto.
***
15. Enyi Mlio amini! Mkikutana na walio kufuru
vitani msiwageuzie mgongo.
***
16. Na atakaye wageuzia mgongo wake siku hiyo
- isipo kuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi - basi atakuwa amestahiki
ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na pahala pake ni Jahannamu, na huo ni mwisho
muovu.
***
17. Hamkuwauwa nyinyi lakini Mwenyezi Mungu ndiye
aliye wauwa. Na wewe hukutupa, walakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye tupa,
ili awajaribu Waumini majaribio mema yatokayo kwake. Hakika Mwenyezi Mungu
ndiye Msikizi na Mjuzi.
***
18. Ndio hivyo! Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kudhoofisha vitimbi vya makafiri.
***
19. Kama mnataka hukumu basi hukumu imekwisha
kujieni. Na mkiacha itakuwa ndio kheri kwenu. Na mkirejea Sisi pia tutarejea.
Na jeshi lenu halitakufaeni kitu, japo likiwa kubwa. Kwani hakika Mwenyezi
yu pamoja na Waumini.
***
20. Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu na
Mtume wake, wala msijiepushe naye, nanyi mnasikia.
***
21. Wala msiwe kama wale wanao sema: Tumesikia,
na kumbe hawasikii.
***
22. Hakika vinyama viovu mbele ya Mwenyezi Mungu
ni vile viziwi na bubu visio tumia akili zao.
***
23. Na Mwenyezi Mungu angeli jua wema wowote kwao
ange wasikilizisha, na lau ange wasikilizisha wangeli geuka wakapuuza.
***
24. Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu
na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele. Na jueni kuwa
Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba hakika kwake
Yeye tu mtakusanywa.
***
25. Na jikingeni na Fitna ambayo haitowasibu walio
dhulumu peke yao kati yenu. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
***
26. Na kumbukeni mlipo kuwa wachache, mkionekana
wanyonge katika nchi, mnaogopa watu wasikunyakueni, naye akakupeni pahala
pazuri pa kukaa, na akakutieni nguvu kwa nusura yake, na akakupeni riziki
nzuri ili mpate kushukuru.
***
27. Enyi mlio amini! Msimfanyie khiana Mwenyezi
Mungu na Mtume, wala msikhini amana zenu, nanyi mnajua.
***
28. Na jueni ya kwamba mali zenu na wana wenu
ni Fitna (mtihani), na kwamba kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa.
***
29. Enyi mlio amini! Mkimcha Mwenyezi Mungu atakupeni
kipambanuo, na atakufutieni makosa, na atakusameheni, na Mwenyezi Mungu
ni Mwenye fadhila kubwa.
***
30. Na walipo kupangia mpango walio kufuru wakufunge,
au wakuuwe, au wakutoe. Wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga
yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa mipango.
***
31. Na wanapo somewa Aya zetu, wao husema: Tumesikia.
Na lau tungeli penda tunge sema kama haya. Haya si chochote ila hadithi
za watu wa kale tu.
***
32. Na walipo sema: Ee Mwenyezi Mungu! Ikiwa haya
ni kweli itokayo kwako basi tunyeshee mawe kutoka mbinguni, au tuletee
adhabu yoyote iliyo chungu.
***
33. Na Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaadhibu nawe
umo pamoja nao, wala Mwenyezi Mungu si wa kuwaadhibu na hali ya kuwa wanaomba
msamaha.
***
34. Lakini wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu
asiwaadhibu, na hali ya kuwa wanawazuilia watu Msikiti Mtakatifu? Wala
wao hawakuwa ndio walinzi wake, bali walinzi wake hawakuwa ila wacha-Mngu
tu. Lakini wengi katika wao hawajui.
***
35. Na haikuwa ibada yao kwenye hiyo Nyumba (Al
Kaaba) ila ni kupiga miunzi na makofi. Basi onjeni adhabu kwa vile mlivyo
kuwa mkikufuru.
***
36. Hakika wale walio kufuru hutoa mali yao ili
kuzuilia Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watayatoa, kisha yatakuwa juu yao
majuto, na kisha watashindwa. Na wale walio kufuru watakusanywa kwenye
Jahannam.
***
37. Ili Mwenyezi Mungu apate kuwa pambanua walio
waovu na walio wema, na kuwaweka waovu juu ya waovu wengine, na kuwarundika
wote pamoja, na kuwatupa katika Jahannam. Hao ndio walio khasirika.
***
38. Waambie wale walio kufuru: Wakikoma watasamehewa
yaliyo kwisha pita. Na wakiyarudia basi imekwisha pita mifano ya wa zamani.
***
39. Na piganeni nao mpaka isiwepo fitna na mateso,
na Dini yote iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Lakini wakiacha, basi hakika
Mwenyezi Mungu anayaona wanayo yatenda.
***
40. Na kama wakigeuka basi jueni kwamba Mwenyezi
Mungu ndiye Mola wenu, ni Mola Mwema na Msaidizi Mwema.
***
41. NA JUENI ya kwamba ngawira mnayo ipata, basi
khums (sehemu moja katika tano) ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume,
na jamaa, na mayatima, na masikini, na wasafiri, ikiwa nyinyi mmemuamini
Mwenyezi Mungu na tuliyo yateremsha kwa mja wetu siku ya kipambanuo, siku
yalipo kutana majeshi mawili. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
***
42. Kumbukeni pale mlipo kuwa nyinyi kwenye ng'ambo
ya karibu ya bonde, na wao wakawa ng'ambo ya mbali, na msafara ulipo kuwa
chini yenu. Na ingeli kuwa mmeagana mngeli khitalifiana katika miadi. Lakini
(mkakutana) ili Mwenyezi Mungu atimize jambo lilio kuwa lazima litendeke,
kwa sababu aangamie wa kuangamia kwa dalili zilizo dhaahiri, na asalimike
wa kusalimika kwa dalili zilizo dhaahiri. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia
Mwenye kujua.
***
43. Kumbuka alipo kuonyesha usingizini mwako kwamba
wao ni wachache - na lau angeli kuonyesha kuwa ni wengi, mngeli ingiwa
na woga, na mngeli zozana katika jambo hilo. Lakini Mwenyezi Mungu kakuvueni.
Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua yalio vifuani.
***
44. Na mlipo kutana akakuonyesheni machoni mwenu
kuwa wao ni wachache, na akakufanyeni nyinyi ni wachache machoni mwao,
ili Mwenyezi Mungu atimize jambo lilio kuwa liwe. Na mambo yote hurejezwa
kwa Mwenyezi Mungu.
***
45. Enyi mlio amini! Mkikutana na jeshi, basi
kueni imara, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufanikiwa.
***
46. Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala
msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika
Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri.
***
47. Wala msiwe kama wale walio toka majumbani
mwao kwa fakhari na kujionyesha kwa watu, na wakawazuilia watu Njia ya
Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ameyazunguka yote wanayo yafanya.
***
48. Na pale Shet'ani alipo wapambia vitendo vyao,
na akawaambia: Hapana watu wa kukushindeni hii leo, na hali mimi ni mlinzi
wenu. Yalipo onana majeshi mawili, akarudi nyuma, na akasema: Mimi si pamoja
nanyi. Mimi naona msiyo yaona. Mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi
Mungu ni mkali wa kuadhibu.
***
49. Na walipo sema wanaafiki, na wale wenye ugonjwa
nyoyoni mwao: Watu hawa dini yao imewadanganya. Na Mwenye kumtegemea Mwenyezi
Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Ametukuka, na Mwenye hikima.
***
50. Na laiti ungeli ona Malaika wanapo wafisha
wale walio kufuru wakiwapiga nyuso zao na migongo yao, na kuwaambia: Ionjeni
adhabu ya Moto!
***
51. Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyo kwisha tangulizwa
na mikono yenu, na hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.
***
52. Kama ada ya watu wa Firauni na walio kuwa
kabla yao - walizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu. Basi Mwenyezi Mungu aliwashika
kwa sababu ya madhambi yao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na
mkali wa kuadhibu.
***
53. Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi
kabisa neema alizo waneemesha watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani
ya nafsi zao. Na hakika Mwwnyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
***
54. Ni kama ada ya watu wa Firauni na walio kabla
yao - walizikanusha Ishara za Mola wao Mlezi, basi tukawateketeza kwa madhambi
yao. Na tukawazamisha watu wa Firauni. Na wote walikuwa wenye kudhulumu.
***
55. Hakika vinyama vilio viovu kabisa mbele ya
Mwenyezi Mungu ni wale wanao kufuru, basi hao hawaamini;
***
56. Wale ambao miongoni mwao umepatana nao ahadi,
kisha wanavunja ahadi yao kila mara, wala hawamchi Mungu.
***
57. Basi ukiwakuta vitani wakimbize walio nyuma
yao ili wapate kukumbuka.
***
58. Na ukichelea khiana kwa watu fulani basi watupilie
ahadi yao kwa usawa. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi makhaini.
***
59. Wala wasidhanie wale walio kufuru kwamba wao
wametangulia mbele. La, wao hawatashinda.
***
60. Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na
kwa farasi walio fungwa tayari-tayari, ili kuwatishia maadui wa Mwenyezi
Mungu na maadui zenu, na wengineo ambao hamwajui, lakini Mwenyezi Mungu
anawajua. Na mkitoa chochote katika Njia ya Mwenyezi Mungu mtarudishiwa,
na wala nyinyi hamtadhulumiwa.
***
61. Na wakielekea amani nawe pia elekea, na mtegemee
Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.
***
62. Na wakitaka kukukhadaa basi Mwenyezi Mungu
atakutosheleza. Kwani Yeye ndiye aliye kuunga mkono kwa nusura yake na
kwa Waumini.
***
63. Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungeli
toa vyote viliomo duniani usingeli weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi
Mungu ndiye aliye waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na
Mwenye hikima.
***
64. Ewe Nabii! Mwenyezi Mungu anakutoshelezea
wewe na Waumini walio kufuata.
***
65. Ewe Nabii! Wahimize Waumini wende vitani.
Wakiwapo kati yenu ishirini wanao subiri watawashinda mia mbili. Na wakiwapo
kati yenu mia watawashinda elfu moja katika walio kufuru. Kwa sababu wao
ni watu wasio fahamu.
***
66. Sasa Mwenyezi Mungu amekupunguzieni, na anajua
kuwa upo udhaifu kwenu. Kwa hivyo wakiwa wapo watu mia moja kati yenu wenye
kusubiri watawashinda mia mbili. Na wakiwapo elfu moja watawashinda elfu
mbili, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye
kusubiri.
***
67. Haimfalii Nabii yeyote kuwa na mateka mpaka
awe ameshinda baraabara katika nchi. Mnataka vitu vya dunia, na Mwenyezi
Mungu anataka Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye
hikima.
***
68. Lau isingeli kuwa hukumu iliyo kwisha tangulia
kutoka kwa Mwenyezi Mungu ingeli kupateni adhabu kubwa kwa vile mlivyo
chukua.
***
69. Basi kuleni katika mlivyo teka, ni halali
na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe
na Mwenye kurehemu.
***
70. Ewe Nabii! Waambie mateka waliomo mikononi
mwenu: Kama Mwenyezi akiona kheri yoyote nyoyoni mwenu atakupeni bora kuliko
vilivyo chukuliwa kwenu, na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe Mwenye kurehemu.
***
71. Ikiwa wanataka kukufanyia khiana, wao walikwisha
mfanyia khiana Mwenyezi Mungu kabla yake, na Yeye akakuwezesha kuwashinda.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
***
72. Hakika wale walio amini na wakahama na wakapigania
Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao, na wale walio toa mahala
pa kukaa, na wakanusuru, hao ni marafiki na walinzi wao kwa wao. Na wale
walio amini lakini hawakuhama, nyinyi hamna waajibu wa ulinzi kwao hata
kidogo mpaka wahame. Lakini wakiomba msaada kwenu katika Dini, basi ni
juu yenu kuwasaidia, isipo kuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu
na wao. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
***
73. Na wale walio kufuru ni marafiki wenyewe kwa
wenyewe. Msipo fanya hivi itakuwako fitna katika nchi na fisadi kubwa.
***
74. Na walio amini wakahama na wakapigana Jihadi
katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na walio toa mahala pa kukaa na wakanusuru,
hao ndio Waumini wa kweli. Watapata msamaha wa Mwenyezi Mungu na kuruzukiwa
kwema.
***
75. Na watakao amini baadaye na wakahajiri, na
wakapigana Jihadi pamoja nanyi, basi hao ni katika nyinyi. Na jamaa wa
nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe zaidi katika Kitabu cha Mwenyezi
Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
***
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com