Hii Sura ya Madina. Idadi za Aya zake ni 120. Na hii ni katika Sura zilizo
shuka karibu na mwisho. Humu umebainishwa waajibu wa kutimiza maagano,
sawa yakiwa baina ya mja na Mola wake Mlezi, au baina ya watu wenyewe kwa
wenyewe. Na Sura hii imebainisha baadhi ya vyakula vilivyo harimishwa,
kama ilivyo bainisha vilivyo halali, na kuhalalisha kuwaoa wanawake wa
Ahlil Kitabi, Wakristo na Mayahudi. Zimetajwa pia humu nguzo za udhu na
kutayamamu. Kadhaalika imeelezwa kutakikana kufanya uadilifu na adui. Na
Sura hii imeashiria neema za Mwenyezi Mungu juu ya Waislamu, na waajibu
wao kukihifadhi Kitabu chao, na ikaelezea kuwa Mayahudi wameyatengua maneno
kutokana na pahala pake, na Wakristo wakayasahau baadhi ya mambo waliyo
kumbushwa, na kwamba wao wamekufuru kwa kusema kwao kuwa Masihi ni mwana
wa Mungu. Kadhaalika Sura hii inawakanusha Mayahudi na Wakristo kwa yale
madai yao kwamba ati wao ni wana wa Mungu na vipenzi vyake. Kisha tena
Sura hii imekusanya baadhi ya khabari za Mayahudi, kama ilivyo kusanya
kisa cha wana wawili wa Adam. Kisa hichi kinathibitisha kuwa uvamizi na
kudhulumiana ni katika tabia za kibinaadamu. Tena kuwajibika kumtoza kisasi
mwenye kudhulumu ni njia ya kuidhibiti tabia hii mbovu isivuke mpaka! Na
Sura Al Maidah imeeleza adhabu ya kumtia adabu mwenye kufanya fiski na
wizi. Tena baadae ikarejea kubainisha vipi Mayahudi walivyo pindua hukumu
za sharia zilizo kuwamo katika Taurati, na ikabainisha kwamba katika Taurati
na Injili ulikuwapo ukweli na haki kabla ya kuchezewa na kugeuzwa geuzwa.
Na ikahakikishwa kuwa ni waajibu kuhukumu kwa mujibu alivyo teremsha Mwenyezi
Mungu. Sura imeashiria juu ya uadui wa Mayahudi na Wakristo kwa Waumini,
na waajibu wa kutowanyenyekea, na kutowaridhia kwa wanayo tenda, na kuwa
ni dharura kuwapinga. Na Sura imethibitisha kuwa Wakristo wamekufuru kwa
kusema kwao Mwenyezi Mungu ni mmoja wa Watatu! Tena Qur'an katika Sura
hii imewasifu baadhi ya Wakristo ambao wameikubali haki na wakaiamini,
na ikamkataza Muumini kujiharimishia mwenyewe vitu vizuri, na ikabainisha
nini kafara ya kuvunja kiapo. Sura hii kadhaalika imeharimisha ulevi kabisa,
na imebainisha ibada za Hija na cheo cha Alkaaba na miezi mitakatifu, na
ikaeleza upotovu wa baadhi ya mambo waliyo jiharimishia Waarabu wenyewe
kwa wenyewe bila ya hoja wala dalili yoyote, kama ilivyo bainisha wasia
wakati wa safari. Mwishoe Sura hii imekhitimisha kwa kutaja miujiza
iliyo tokea kwa Nabii Isa a.s. Na juu ya hiyo miujiza Banu Israili walimkanya.
Pia Sura imetaja kuwa Nabii Isa a.s. hana dhambi ya walio potoka wakamuabudu,
na imeeleza Ufalme wa Mwenyezi Mungu Subhanahu juu ya mbingu na ardhi,
na ukamilifu wa uwezo wake.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU, MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Enyi mlio amini! Timizeni ahadi. Mmehalalishiwa
wanyama wa mifugo, ila wale mnao tajiwa. Lakini msihalalishe kuwinda nanyi
mmo katika Hija. Hakika Mwenyezi Mungu anahukumu apendavyo.
***
2. Enyi mlio amini! Msivunje hishima ya alama ya
Dini ya Mwenyezi Mungu wala mwezi mtakatifu, wala wanyama wanao pelekwa
Makka kuchinjwa, wala vigwe vyao, wala wanao elekea kwendea Nyumba Takatifu,
wakitafuta fadhila na radhi za Mola wao Mlezi. Na mkisha toka Hija yenu
basi windeni. Wala kuwachukia watu kwa kuwa wali- kuzuilieni kufika Msikiti
mtakatifu kusikupelekeeni kuwafanyia uadui. Na saidianeni katika wema na
uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu. ***
3. Mmeharimishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya
nguruwe, na mnyama aliye chinjwa si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na aliye
kufa kwa kunyongeka koo, na aliye kufa kwa kupigwa, na aliye kufa kwa kuanguka,
na aliye kufa kwa kupigwa pembe, aliye liwa na mnyama, ila mkimdiriki kumchinja.
Na pia ni haramu kula nyama aliye chinjiwa masanamu. Na ni haramu kupiga
ramli. Hayo yote ni upotovu. Leo walio kufuru wamekata tamaa na Dini yenu;
basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi. Leo nimekukamiliishieni Dini yenu,
na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini.
Na mwenye kushurutishwa na njaa, bila ya kupendelea dhambi, basi hakika
Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kurehemu. ***
4. Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema: Mmehalalishiwa
kila vilivyo vizuri na mlicho wafundisha wanyama kukiwinda. Mnawafundisha
alivyo kufunzeni Mwenyezi Mungu. Basi kuleni walicho kukamatieni, na mkisomee
jina la Mwenyezi Mungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwepesi wa kuhisabu. ***
5. Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula
cha walio pewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao.
Na pia wanawake wema miongoni mwa Waumini, na wanawake wema miongoni mwa
walio pewa Kitabu kabla yenu, mtakapo wapa mahari yao, mkafunga nao ndoa,
bila ya kufanya uhasharati wala kuwaweka kinyumba. Na anaye kataa kuamini
bila shaka a'mali yake imepotea, naye katika Akhera atakuwa miongoni mwa
wenye khasara. ***
6. Enyi mlio amini! Mnapo simama kwa ajili ya Sala
basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa
vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni.
Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa
wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake
nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu;
bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru.
***
7. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu
yenu, na ahadi yake aliyo fungamana nanyi mlipo sema: Tumesikia na tumet'ii.
Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi sana wa yaliyomo
vifuani. ***
8. Enyi mlio amini! Kuweni wasimamizi madhubuti
kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na
watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa
karibu mno na uchamngu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu
anazo khabari za mnayo yatenda. ***
9. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio muamini na wakatenda
mema kwamba watapata maghfira na malipo makubwa. ***
10. Na wale walio kufuru na wakakanusha Ishara
zetu, hao ndio watu wa Motoni. ***
11. Enyi mlio amini! Kumbukeni neema za Mwenyezi
Mungu zilizo juu yenu, walipo taka watu kukunyooshieni mikono, naye akaizuilia
mikono yao kukufikieni. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Waumini wamtegemee
Mwenyezi Mungu tu. ***
12. Na Mwenyezi Mungu alifanya agano na Wana wa
Israili. Na tukawateulia kutokana nao wakuu kumi na mbili. Na Mwenyezi
Mungu akasema: Kwa yakini Mimi ni pamoja nanyi. Mkisali, na mkatoa Zaka,
na mkawaamini Mitume wangu, na mkawasaidia, na mkamkopesha Mwenyezi Mungu
mkopo mwema, hapana shaka nitakufutieni maovu yenu na nitakuingizeni katika
mabustani yapitayo mito kati yake. Lakini atakaye kufuru miongoni mwenu
baada ya hayo bila ya shaka atakuwa amepotea njia iliyo sawa. ***
13. Basi kwa sababu ya kuvunja agano lao tuliwalaani,
na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu. Wanayabadilisha maneno kutoka pahala
pake, na wamesahau sehemu ya yale waliyo kumbushwa. Na huachi kuvumbua
khiana kutokana nao, isipo kuwa wachache miongoni mwao. Basi wasamehe na
waache. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema. ***
14. Na kutoka kwa wale walio sema: Sisi ni Manasara,
tulichukua ahadi yao, lakini wakasahau sehemu ya waliyo kumbushwa. Kwa
hivyo tukaweka kati yao uadui na chuki mpaka Siku ya Kiyama. Na hapo Mwenyezi
Mungu atawaambia waliyo kuwa wakiyafanya. ***
15. Enyi Watu wa Kitabu! Amekwisha kujieni Mtume
wetu anaye kufichulieni mengi mliyo kuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anaye
samehe mengi. Bila shaka imekujieni kutoka kwa Mwenyezi Mungu nuru na Kitabu
kinacho bainisha. ***
16. Mwenyezi Mungu huwaongoa wenye kufuata radhi
yake katika njia za salama, na huwatoa katika giza kuwapeleka kwenye nuru
kwa amri yake, na huwaongoa kwenye njia iliyo nyooka. ***
17. Hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu
ni Masihi mwana wa Maryamu. Sema: Ni nani mwenye kumiliki cho chote mbele
ya Mwenyezi Mungu ikiwa Yeye angetaka kumuangamiza Masihi mwana wa Maryamu,
na mama yake, na wote waliomo katika ardhi? Na mamlaka ya mbingu na ardhi
na vilivyomo ndani yake ni vya Mwenyezi Mungu. Huumba apendavyo. Na Mwenyezi
Mungu anao uweza juu ya kila kitu. ***
18. Na Mayahudi na Wakristo wanasema: Sisi ni
wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake. Sema: Basi kwa nini anakuadhibuni
kwa ajili ya dhambi zenu? Bali nyinyi ni watu tu kama wale wengine alio
waumba. Humsamehe amtakaye na humuadhibu amtakaye. Na ni wa Mwenyezi Mungu
tu ufalme wa mbingu na ardhi. Na marejeo ni kwake Yeye. ***
19. Enyi Watu wa Kitabu! Bila ya shaka amekujilieni
Mtume wetu akikubainishieni katika wakati usio kuwa na Mitume, msije mkasema:
Hakufika kwetu mbashiri wala mwonyaji. Basi amekujieni mbashiri na mwonyaji.
Na Mwenyezi Mungu anao uweza wa kila kitu. ***
20. Na pale Musa alipo waambia watu wake: Enyi
watu wangu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, alipo wateuwa
Manabii kati yenu, na akakufanyeni watawala, na akakupeni ambayo hakuwapa
wowote katika walimwengu. ***
21. Enyi watu wangu! Ingieni katika nchi takatifu
ambayo Mwenyezi Mungu amekuandikieni. Wala msirudi nyuma, msije mkawa wenye
kukhasirika. ***
22. Wakasema: Ewe Musa! Huko wako watu majabari.
Nasi hatutaingia huko mpaka wao watoke humo. Wakitoka humo hapo tutaingia.
***
23. Watu wawili miongoni mwa wachamngu ambao Mwenyezi
Mungu amewaneemesha, walisema: Waingilieni kwa mlangoni. Mtakapo waingilia
basi kwa yakini nyinyi mtashinda. Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi
ni Waumini. ***
24. Wakasema: Ewe Musa! Sisi hatutaingia humo
kamwe maadamu wao wamo humo. Basi nenda wewe na Mola wako Mlezi mkapigane.
Sisi tutakaa hapa hapa. ***
25. Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi similiki
ila nafsi yangu na ndugu yangu. Basi tutenge na hawa watu wapotovu.
***
26.(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi nchi hiyo wameharimishiwa
muda wa miaka arubaini, watakuwa wakitanga-tanga katika ardhi. Basi wewe
usiwasikitikie watu wapotovu. ***
27. Na wasomee khabari za wana wawili wa Adam
kwa kweli. Walipo toa mhanga, ukakubaliwa wa mmoja wao, na wa mwengine
haukukubaliwa. Akasema: Nitakuuwa. Akasema mwengine: Mwenyezi Mungu huwapokelea
wachamngu. ***
28.Ukininyooshea mkono wako kuniuwa, mimi sitakunyooshea
mkono wangu kukuuwa. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu
wote. ***
29. Mimi nataka ubebe dhambi zangu na dhambi zako,
kwani wewe utakuwa miongoni mwa watu wa Motoni. Na hayo ndiyo malipo ya
wenye kudhulumu. ***
30. Basi nafsi yake ikampelekea kumuuwa nduguye,
akamuuwa na akawa miongoni mwa wenye kukhasirika. ***
31. Hapo Mwenyezi Mungu akamleta kunguru anaye
fukua katika ardhi ili amwonyeshe vipi kumsitiri nduguye. Akasema: Ole
wangu! Nimeshindwa kuwa kama kunguru huyu nikamsitiri ndugu yangu? Basi
akawa miongoni mwa wenye kujuta. ***
32. Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili
ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika
nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti
ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo
wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi.
***
33.Basi malipo ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi
Mungu na Mtume wake na wakawania kufanya uchafuzi katika nchi, ni kuuwawa,
au kusalibiwa, au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa
nchi. Hii ndiyo hizaya yao katika dunia; na katika Akhera watapata adhabu
kubwa. ***
34. Isipo kuwa wale walio tubu kabla hamjawatia
nguvuni. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.
***
35. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na
tafuteni njia ya kumfikilia. Na wanieni kwa juhudi kwa ajili yake ili mpate
kuokoka. ***
36. Hakika walio kufuru lau wange kuwa na yote
yaliyomo duniani, na mengine kama hayo, ili watoe fidia ya kuepukana na
adhabu ya Siku ya Kiyama, yasingeli pokelewa kwao; na watapata adhabu chungu.
***
37. Watataka watoke Motoni, lakini hawatatoka
humo, na watakuwa na adhabu inayo dumu. ***
38. Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni
mikono yao, hayo ni malipo ya waliyo yachuma, ndiyo adhabu ya mfano itokayo
kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
***
39. Lakini mwenye kutubia baada ya dhulma yake,
na akatengenea, basi Mwenyezi Mungu atapokea toba yake. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu. ***
40. Hujui ya kwamba Mwenyezi Mungu anao ufalme
wa mbingu na ardhi? Humuadhibu amtakaye, na humsamehe amtakaye. Na Mwenyezi
Mungu ni Muweza wa kila kitu. ***
41. Ewe Mtume! Wasikuhuzunishe wa fanyao haraka
kukufuru, miongoni mwa wanao sema kwa vinywa vyao: Tumeamini, na hali nyoyo
zao hazikuamini, na miongoni mwa Mayahudi, wanao sikiliza kwa ajili ya
uwongo, wanao sikiliza kwa ajili ya watu wengine wasio kufikia. Wao huyabadilisha
maneno kutoka pahala pake. Wanasema: Mkipewa haya basi yashikeni, na msipo
pewa haya tahadharini. Na mtu ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumfitini huwezi
kuwa na madaraka naye mbele ya Mwenyezi Mungu. Hao ndio ambao Mwenyezi
Mungu hataki kuzitakasa nyoyo zao. Watakuwa na hizaya duniani, na Akhera
watakuwa na adhabu kubwa. ***
42. Hao ni wasikilizaji kwa ajili ya kusema uwongo,
na ni walaji mno vya haramu! Basi wakikujia, wahukumu baina yao au jipuuze
nao. Na ukijipuuza nao, basi wao hawatakudhuru kitu. Na ukiwahukumu, basi
hukumu baina yao kwa uadilifu. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda waadilifu.
***
43. Na huwaje wakufanye wewe hakimu nao wanayo
Taurati yenye hukumu za Mwenyezi Mungu? Kisha baada ya hayo wanageuka.
Na hao si wenye kuamini. ***
44. Hakika Sisi tuliteremsha Taurati yenye uwongofu
na nuru, ambayo kwayo Manabii walio nyenyekea kiislamu, na wachamngu, na
wanazuoni, waliwahukumu Mayahudi; kwani walikabidhiwa kukihifadhi Kitabu
cha Mwenyezi Mungu. Nao wakawa ni mashahidi juu yake. Basi msiwaogope watu,
bali niogopeni Mimi. Wala msibadilishe Aya zangu kwa thamani chache. Na
wasio hukumu kwa aliyo teremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri.
***
45. Na humo tuliwaandikia ya kwamba roho kwa roho,
na jicho kwa jicho, na pua kwa pua, na sikio kwa sikio, na jino kwa jino,
na kwa majaraha kisasi. Lakini atakaye samehe basi itakuwa ni kafara kwake.
Na wasio hukumu kwa yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio
madhaalimu. ***
46. Na tukawafuatishia hao Isa bin Maryamu kuyahakikisha
yaliyo kuwa kabla yake katika Taurati, na tukampa Injili iliyomo ndani
yake uwongofu, na nuru na inayo sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika
Taurati, na uwongofu na mawaidha kwa wachamngu. ***
47. Na wahukumu Watu wa Injili kwa yale aliyo
teremsha Mwenyezi Mungu ndani yake. Na wasio hukumu kwa yale aliyo yateremsha
Mwenyezi Mungu basi hao ndio wapotofu. ***
48. Na tumekuteremshia wewe, kwa haki, Kitabu
hichi kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda.
Basi hukumu baina yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate
matamanio yao ukaacha Haki iliyo kujia. Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea
sharia yake na njia yake. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka ange kufanyeni
nyote umma mmoja, lakini ni kukujaribuni kwa aliyo kupeni. Basi shindaneni
kwa mambo ya kheri. Kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo yenu nyote, na atakuja
kuwaambieni yale mliyo kuwa mkikhitalifiana. ***
49. Na wahukumu baina yao kwa aliyo yateremsha
Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao. Nawe tahadhari nao wasije
kukufitini ukaacha baadhi ya aliyo kuteremshia Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka,
basi jua kwamba hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwasibu kwa baadhi ya dhambi
zao. Na hakika wengi wa watu ni wapotofu. ***
50. Je, wao wanataka hukumu za Kijahiliya? Na
nani aliye mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu kwa watu wenye
yakini? ***
51. Enyi mlio amini! Msiwafanye Mayahudi na Wakristo
kuwa ni marafiki. Wao ni marafiki wao kwa wao. Na miongoni mwenu mwenye
kufanya urafiki nao, basi huyo ni katika wao. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi
watu wenye kudhulumu. ***
52. Utawaona wale wenye maradhi nyoyoni mwao wanakimbilia
kwao wakisema: Tunakhofu yasitusibu mabadiliko. Huenda Mwenyezi Mungu akaleta
ushindi au jambo jingine litokalo kwake wakawa wenye kujuta kwa waliyo
yaficha katika nafsi zao. ***
53. Na walio amini watasema: Hivyo hawa ndio wale
walio apa ukomo wa viapo vyao kuwa wao wa pamoja nanyi? Vitendo vyao vitapotea
bure, na wataamkia kuwa wenye kukhasirika. ***
54. Enyi mlio amini! Atakaye iacha miongoni mwenu
Dini yake, basi Mwenyezi Mungu atakuja leta watu anao wapenda nao wanampenda,
wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu juu ya makafiri, wanapigania Jihadi
katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama ya anaye laumu. Hiyo
ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu
na Mwenye kujua. ***
55. Hakika rafiki yenu mlinzi ni Mwenyezi Mungu
na Mtume wake na walio amini, ambao hushika Sala na hutoa Zaka nao wananyenyekea.
***
56. Na atakaye fanya urafiki na Mwenyezi Mungu
na Mtume wake na walio amini, basi hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo
lenye kushinda. ***
57. Enyi mlio amini! Msiwafanye marafiki wale
walio ifanyia kejeli na mchezo Dini yenu miongoni mwa walio pewa Kitabu
kabla yenu, na makafiri wengine. Na mcheni Mwenyezi Mungu kama nyinyi ni
wenye kuamini. ***
58. Na mnapo adhinia Sala wao wanaichukulia maskhara
na mchezo. Hayo ni kwa sababu wao ni watu wasio na akili. ***
59. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Hivyo mnatuchukia
kwa kuwa tumemuamini Mwenyezi Mungu na tuliyo teremshiwa na yaliyo teremshwa
kabla, na kwa kuwa wengi katika nyinyi ni wapotofu? ***
60. Sema: Je! Nikwambieni yule ambaye ni mwenye
malipo mabaya zaidi kuliko hayo mbele ya Mwenyezi Mungu? Ni yule ambaye
Mwenyezi Mungu amemlaani na amemkasirikia, na amewafanya miongoni mwao
manyani na nguruwe, na wakamuabudu Shet'ani. Hao ndio wenye mahali pabaya
na wamepotea zaidi njia iliyo sawa. ***
61. Na wanapo kujieni husema: Tumeamini. Lakini
hakika wao wameingia na ukafiri wao, na wametoka nao pia. Na Mwenyezi Mungu
ni Mjuzi kabisa wa yote wanayo yaficha. ***
62. Na utawaona wengi katika wao wanakimbilia
kwenye dhambi, na uadui, na ulaji wao vya haramu. Ni maovu mno hayo wayatendayo!
***
63. Mbona hao wanazuoni na makohani wao hawawakatazi
maneno yao ya dhambi, na ulaji wao vya haramu? Ni maovu mno hayo wayafanyayo!
***
64. Na Mayahudi walisema: Mkono wa Mwenyezi Mungu
umefumba. Mikono yao ndiyo iliyo fumba, na wamelaaniwa kwa sababu ya waliyo
yasema. Bali mikono yake iwazi. Hutoa apendavyo. Kwa yakini yaliyo teremshwa
kwako kutoka kwa Mola wako Mlezi yatawazidisha wengi katika wao uasi na
kufuru. Na Sisi tumewatilia uadui na chuki baina yao mpaka Siku ya Kiyama.
Kila mara wanapo washa moto wa vita, Mwenyezi Mungu anauzima. Na wanajitahidi
kuleta uharibifu katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi waharibifu.
***
65. Na lau kuwa Watu wa Kitabu wangeli amini na
wakachamngu hapana shaka tungeli wafutia makosa yao, na tungeli waingiza
katika Bustani zenye neema. ***
66. Na lau kuwa wangeli ishika Taurati na Injili
na yote waliyo teremshiwa kutokana na Mola wao Mlezi, basi hapana shaka
wangeli kula vya juu yao na vya chini ya miguu yao. Wapo watu miongoni
mwao walio sawa, lakini wengi wao wanayo yafanya ni mabaya mno. ***
67. Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka
kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake.
Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
makafiri. ***
68. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Hamna lenu jambo
mpaka muishike Taurati na Injili na yote mlio teremshiwa kutokana na Mola
wenu Mlezi. Na hakika ulio teremshiwa wewe kutokana na Mola wako Mlezi
yatawazidishia wengi katika wao uasi na ukafiri. Basi usiwasikitikie watu
makafiri. ***
69. Hakika walio amini, na Mayahudi na Masabii
na Wakristo, walio muamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya mwisho, na wakatenda
mema, basi hawatakuwa na khofu wala hawatahuzunika. ***
70. Tulifanya agano na Wana wa Israili, na tukawatumia
Mitume. Kila alipo wajia Mtume kwa wasio yapenda nafsi zao wengine waliwakanusha
na wengine wakawauwa. ***
71. Na wakadhani kuwa hapatakuwa majaribio; basi
wakawa vipofu na viziwi. Kisha Mwenyezi Mungu akawapokelea toba zao. Kisha
tena wengi katika wao wakawa vipofu na viziwi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kuyaona hayo wayatendayo. ***
72. Hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryamu! Na hali Masihi mwenyewe alisema: Enyi Wana wa Israili! Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Kwani anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na walio dhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru. ***
73. Kwa hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi
Mungu ni wa tatu wa Utatu. Hali hakuna mungu ila Mungu Mmoja. Na ikiwa
hawaachi hayo wanayo yasema, kwa yakini itawakamata adhabu chungu wale
wanao kufuru. ***
74. Je! Hawatubu kwa Mwenyezi Mungu na wakamwomba
msamaha? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu. ***
75. Masihi mwana wa Maryam si chochote ila ni
Mtume. Wamekwisha pita Mitume kabla yake. Na mama yake ni mwanamke mkweli.
Wote wawili walikuwa wakila chakula. Angalia jinsi tunavyo wabainishia
Aya, kisha angalia vipi wanavyo geuzwa. ***
76. Sema: Je! Mnawaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu,
wale ambao hawawezi kukudhuruni wala kukufaeni? Na Mwenyezi Mungu ndiye
Mwenye kusikia, Mwenye kujua. ***
77. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika
dini yenu bila ya haki. Wala msifuate matamanio ya watu walio kwisha potea
tangu zamani, na wakawapoteza wengi, na wenyewe wakapotea njia iliyo sawa.
***
78. Walilaaniwa walio kufuru miongoni mwa Wana
wa Israili kwa ulimi wa Daud na wa Isa mwana wa Maryamu. Hayo ni kwa sababu
waliasi na wakawa wanapindukia mipaka. ***
79. Walikuwa hawakatazani maovu waliyo kuwa wakiyafanya.
Hakika ni maovu yalioje mambo waliyo kuwa wakiyafanya! ***
80. Utawaona wengi wao wanafanya urafiki na walio
kufuru. Hakika ni maovu yaliyo tangulizwa na nafsi zao hata Mwenyezi Mungu
amewakasirikia, nao watadumu katika adhabu. ***
81. Na lau wangeli kuwa wanamuamini Mwenyezi Mungu,
na huyu Nabii, na yaliyo teremshwa kwake, wasingeli wafanya hao marafiki.
Lakini wengi katika wao ni wapotofu. ***
82. Hakika utawakuta walio shadidi kuliko watu
wote katika uadui kwa walio amini ni Mayahudi na washirikina. Na utawakuta
walio karibu mno kwa mapenzi ni wale wanao sema: Sisi ni Manasara. Hayo
ni kwa sababu wapo miongoni mwao makasisi na wamonaki, na kwa sababu wao
hawafanyi kiburi. ***
83. NA WANAPO SIKIA yaliyo teremshwa kwa Mtume
utaona macho yao yanachururika machozi kwa sababu ya Haki waliyo itambua.
Wanasema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini. Basi tuandike pamoja na wanao shuhudia.
***
84. Na kwa nini tusimuamini Mwenyezi Mungu na
Haki iliyo tujia, na hali tunatumai Mola wetu Mlezi atuingize pamoja na
watu wema? ***
85. Basi Mwenyezi Mungu atawalipa, kwa yale waliyo
yasema, Bustani zipitazo mito katika yake; humo watadumu. Na haya ndiyo
malipo ya wafanyao wema. ***
86. Na wale walio kufuru na wakazikanusha Ishara
zetu, hao ndio watu wa Motoni. ***
87. Enyi mlio amini! Msiharimishe vizuri alivyo
kuhalalishieni Mwenyezi Mungu, wala msikiuke mipaka. Hakika Mwenyezi Mungu
hawapendi wakiukao mipaka. ***
88. Na kuleni katika alivyo kuruzukuni Mwenyezi
Mungu, halali na vizuri. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini.
***
89. Mwenyezi Mungu hatakushikeni kwa viapo vyenu
vya upuuzi, lakini atakushikeni kwa mnavyo apa kweli kweli kwa makusudio.
Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho
walisha ahali zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Asiye pata hayo,
basi afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapo apa. Na hifadhini
yamini zenu. Namna hivyo Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake ili mpate
kushukuru. ***
90. Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na kamari,
na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet'ani.
Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa. ***
91. Hakika Shet'ani anataka kutia kati yenu uadui
na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na
kusali. Basi je, mmeacha? ***
92. Na mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume,
na tahadharini. Na ikiwa mtageuka basi jueni ya kuwa juu ya Mtume wetu
ni kufikisha ujumbe tu ulio wazi. ***
93. Si dhambi juu ya walio amini na wakatenda
mema kwa walivyo vila (zamani) maadamu wakichamngu na wakiamini na wakitenda
mema, kisha wakachamngu, na wakaamini, kisha wakachamngu na wakafanya mazuri.
Na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao mazuri. ***
94. Enyi mlio amini! Mwenyezi Mungu atakujaribuni
kidogo kwa wanyama wa kuwinda inayo wafikia mikono yenu na mikuki yenu,
ili Mwenyezi Mungu amjue nani anaye mkhofu kwa ghaibu. Basi atakaye ruka
mipaka baada ya hayo atapata adhabu kali. ***
95. Enyi mlio amini! Msiue wanyama wa kuwinda
nanyi mmeharimia katika Hija. Na miongoni mwenu atakaye muuwa makusudi,
basi malipo yake yatakuwa kwa kuchinja kilicho sawa na alicho kiuwa, katika
mifugo, kama wanavyo hukumu waadilifu wawili miongoni mwenu. Mnyama huyo
apelekwe kwenye Al Kaaba, au kutoa kafara kwa kuwalisha masikini; au badala
ya hayo ni kufunga, ili aonje ubaya wa jambo lake hili. Mwenyezi Mungu
amekwisha yafuta yaliyo pita; lakini atakaye fanya tena Mwenyezi Mungu
atampa adhabu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu na Mwenye kuadhibu.
***
96. Nyinyi mmehalalishiwa kuvua vinyama vya baharini
na kuvila, kwa faida yenu na kwa wasafiri. Na mmeharimishiwa mawindo ya
wanyama wa bara maadamu mmeharimia Hija. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye
mtakusanywa kwake. ***
97. Mwenyezi Mungu ameifanya Al Kaaba, hii Nyumba
Tukufu, ni simamio la watu, na kadhaalika Miezi Mitukufu, na wanyama wa
dhabihu, na vigwe. Hayo ili mjue ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo
mbinguni na yaliyomo katika ardhi, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi
wa kila kitu. ***
98. Jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu,
na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, na Mwenye kurehemu.
***
99. Haimlazimu Mtume ila kufikisha ujumbe tu.
Na Mwenyezi Mungu anajua mnacho kidhihirisha na mnacho kificha. ***
100. Sema: Haviwi sawa viovu na vyema ujapo kupendeza
wingi wa viovu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, enyi wenye akili, ili mpate
kufanikiwa. ***
101. Enyi mlio amini! Msiulize mambo ambayo mkidhihirishiwa
yatakuchukizeni. Na mkiyauliza inapo teremshwa Qur'ani mtabainishiwa. Mwenyezi
Mungu amesamehe hayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira Mpole. ***
102. Waliyauliza hayo watu wa kabla yenu, kisha
wakawa wenye kuyakataa. ***
103. Mwenyezi Mungu hakujaalia uharamu wowote
juu ya "Bahira" wala "Saiba" wala "Wasila" wala "Hami". Lakini walio kufuru
humzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na wengi wao hawatumii akili. ***
104. Na wanapo ambiwa: Njooni kwenye yale aliyo
yateremsha Mwenyezi Mungu, na kwa Mtume, husema: Yanatutosha tuliyo wakuta
nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawajui kitu wala hawakuongoka?
***
105. Enyi mlio amini! Kilicho lazima juu yenu
ni nafsi zenu. Hawakudhuruni walio potoka ikiwa nyinyi mmeongoka. Ni kwa
Mwenyezi Mungu ndio marudio yenu nyote; basi atakwambieni yale mliyo kuwa
mkiyatenda. ***
106. Enyi mlio amini! Yanapo mfikia mauti mmoja
wenu na akataka kutoa wasia, basi wawepo mashahidi wawili miongoni mwenu
ambao ni waadilifu. Na mnapo kuwa safarini, na msiba wa mauti ukakusibuni,
basi washuhudie wengineo wawili wasio kuwa katika nyinyi. Mtawazuia wawili
hao baada ya Sala na waape kwa Mwenyezi Mungu, mkitilia shaka, wakisema:
Hatutopokea thamani yoyote kwa haya hata kwa ajili ya jamaa; na wala hatutaficha
ushahidi wa Mwenyezi Mungu; hakika hapo tutakuwa miongoni mwa wenye dhambi.
***
107.Ikigundulikana kuwa wawili hao wamestahiki
dhambi, basi wawili wengineo kutokana na warithi wenye kudai haki washike
makamo ya wa mwanzo. Nao waape kwa Mwenyezi Mungu wakisema: Hakika ushahidi
wetu ni wa haki zaidi kuliko ushahidi wa wale. Na sisi hatujafanya dhambi;
hakika hapo tutakuwa miongoni mwa walio dhulumu. ***
108. Hivi inaelekea zaidi ya kwamba watatoa ushahidi
ulio sawa au wataogopa visije vikaletwa viapo vingine baada ya viapo vyao.
Na mcheni Mwenyezi Mungu na msikie. Na hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi
wapotofu. ***
109. Ile siku ambayo Mwenyezi Mungu atapo wakusanya
Mitume awaambie: Mlijibiwa nini? Watasema: Hatuna ujuzi; hakika Wewe ndiye
Mjuzi Mkubwa wa yote yaliyo fichikana. ***
110. Na pale Mwenyezi Mungu atapo sema: Ewe Isa
bin Maryamu! Kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipo
kutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na watu katika utoto na utuuzimani.
Na nilivyo kufunza kuandika na hikima na Taurati na Injili. Na ulipo tengeneza
udongo sura ya ndege, kwa idhini yangu, kisha ukapuliza ikawa ndege kwa
idhini yangu; na ulipo waponesha vipofu na wakoma kwa idhini yangu; na
ulipo wafufua wafu kwa idhini yangu; na nilipo kukinga na Wana wa Israili
ulipo wajia na hoja zilizo wazi, na wakasema walio kufuru miongoni mwao:
Haya si lolote ila ni uchawi mtupu! ***
111. Na nilipo wafunulia Wanafunzi kwamba waniamini
Mimi na Mtume wangu, wakasema: Tumeamini na shuhudia kuwa sisi ni Waislamu.
***
112. Wanafunzi walipo sema: Ewe Isa bin Maryamu!
Je, Mola wako Mlezi anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni? Akasema:
Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini. ***
113. Wakasema: Tunataka kukila chakula hicho,
na nyoyo zetu zitue, na tujue kwamba umetuambia kweli, na tuwe miongoni
mwa wanao shuhudia. ***
114. Akasema Isa bin Maryamu: Ewe Mwenyezi Mungu,
Mola Mlezi wetu! Tuteremshia chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa
ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni Ishara itokayo kwako.
Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanao ruzuku. ***
115. Mwenyezi Mungu akasema: Hakika Mimi nitakuteremshieni
hicho. Lakini yeyote katika nyinyi atakaye kanya baadae, basi hakika Mimi
nitampa adhabu nisiyopata kumpa yeyote katika walimwengu. ***
116. Na pale Mwenyezi Mungu atakapo sema: Ewe
Isa bin Maryamu! Ati wewe uliwaambia watu: Nifanyeni mimi na mama yangu
kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu? (Na Isa) atasema: Subhanaka, Wewe
umetakasika! Hainifalii mimi kusema ambayo si haki yangu. Ikiwa nilisema
basi bila ya shaka umekwisha yajua. Wewe unayajua yaliyo ndani ya nafsi
yangu, lakini mimi siyajui yaliyo katika nafsi yako. Hakika Wewe ndiye
Mjuzi mkubwa wa yaliyo fichikana. ***
117. Sikuwaambia lolote ila uliyo niamrisha,
nayo ni: Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi.
Na mimi nilikuwa shahidi juu yao nilipo kuwa nao. Na ulipo nifisha ukawa
Wewe ndiye Muangalizi juu yao. Na Wewe ni shahidi juu ya kila kitu.
***
118. Ukiwaadhibu basi hao ni waja wako. Na ukiwasamehe
basi Wewe ndiye Mwenye nguvu na Mwenye hikima. ***
119. Mwenyezi Mungu atasema: Hii ndiyo Siku ambayo
wasemao kweli utawafaa ukweli wao. Wao watapata Bustani zipitazo mito kati
yake. Humo watadumu milele. Mwenyezi Mungu amewawia radhi, nao wawe radhi
naye. Huku ndiko kufuzu kukubwa. ***
120. Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye ufalme wa mbingu
na ardhi na vilivyomo. Naye ni Muweza wa kila kitu. ***
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com